1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Haki na maridhiano ndiyo njia pekee ya kuiponya Syria

Mohammed Khelef
15 Machi 2021

Miaka kumi baada ya Wasyria kuthubutu kuota ndoto ya kuishi kwa heshima na uhuru, madhara ya ndoto yao hiyo yamefurutu ada, na sasa Maissun Melhem wa DW, ambaye mwenyewe ni Msyria, anasema ni haki pekee ya kuitibu nchi.

https://p.dw.com/p/3qenv
BG Photos and testimonies from Syrian photographers |  Bassam Khabieh
Picha: Bassam Khabieh/OCHA

Mwaka 2020, pale sherehe zilipokuwa zikiwezekana, na watengenezaji na wachezaji filamu walipokuwa wanaweza kukutana kwenye Tuzo za Academy mjini Los Angeles, Wasyria wengi walikuwa na sababu ya kushangiria. 

Filamu mbili kutoka Syria zilikuwa zimeteuliwa kwa kuwa bora kabisa. Moja ni ile iliyoitwa Pango, ambayo ilihusu hospitali ya chini ya ardhi katika kiunga cha Ghoutha kilicho karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus. Hospitali hiyo ilikuwa ikiendeshwa na kikosi cha madaktari wa kike ambao walikuwa wakiwatibu wahanga wa mashambulizi ya anga ya serikali. 

Filamu  nyengine ni Kwa Ajili ya Sama, ambayo iliongozwa na washindi wa Tuzo ya Emmy, Waad al-Kateab na Edward Watts, ikizungumzia kuzingirwa kwa mji wa Aleppo kwa zaidi ya miaka mitano na vikosi vya serikali. 

Waad aliyekanyaga zulia jekundu akiwa na binti yake Sama aliyepewa jina la filamu hiyo, alipata umashuhuri kwa kanzu yake aliyovaa ikiwa na maandishi ya Kiarabu yenye maana ya "Tuliota ndoto, na hatutajutia heshima yetu." 

DW Quadriga - Gast Melhem, Maissun
Maissun Melhem wa DWPicha: DW

Sentensi hii imekuja kugeuka kuwa kaulimbiu ya Wasyria wanaokumbuka miaka 10 ya jaribio lao la mapinduzi dhidi ya utawala wa kikatili kabisa na kidikteta katika zama hizi. Ninapoangalia haya na kukumbuka taswira za kuogofya za muongo huu mmoja uliopita, huwa najiuliza mwenyewe: Je ni kweli hatujutii?

Mambo yalivyoanza

Majira ya Kiangazi ya mwaka 2011 yalikuwa yamejaa matumaini. Kilichoitwa Machipuko ya Arabuni, kumaanisha wimbi la maandamano ya umma dhidi ya tawala za kikandamizaji, lilikuwa linaonekana kuzaa matunda. 

Tawala za kidikteta zilizokuwa zimedumu kwa miongo kadhaa zilianza kuporomoka kutokana na shinikizo kubwa la maandamano ya amani mitaani na kwenye mitandao ya kijamii. Vuguvugu hilo likawatia hamasa wanafunzi wadogo mjini Daraa ambao waliandika kwenye ukuta wa skuli yao: "Ni damu yako, Dokta" jina ambalo huwa anaitwa Bashar al-Assad aliyesomea udaktari nchini Uingereza na kisha kurithi urais kutoka kwa baba yake, Hafidh al-Assad. 

Watoto hao wakakamatwa na kuteswa, na punde wimbi la maandamano likaenea nchi nzima na hata kwa Wasyria wanaoishi nje. Waandamanaji hao walikuwa na mauwa mikononi na huku wakipiga mayowe ya kudai uhuru na heshima. Halikuwa vuguvugu la kisiasa, bali linalozungumzia masuala ya kijamii na lilichochea mitindo mipya ya sanaa na hadithi nyingi za mapenzi. Lilikuwa na dira ya ukubalifu na ujumuishaji wa kila mmoja. Ilikuwa aina fulani ya kiangazi cha mapenzi cha Syria.

Mtoto wangu wa kiume ni zao la kiangazi hiki cha mapenzi cha Syria. Nilipomzaa, sio tu kwamba umama ulinifanya kuuaga ujana wa miaka yangu 20 kwa mabusu, bali pia ulifanikiwa kuihamisha akili yangu kutoka lindi la huzuni za kwetu. 

Machungu yaliyowasibu Wasyria

Machungu waliyosababishiwa Wasyria ni mengi: kuanzia risasi za moto dhidi ya waandamanaji, hadi mabomu ya matangi na makombora ya Scud na hadi kemikali za sumu dhidi ya kiunga kizima, kulikopelekea raia 1,300 kupoteza maisha kwa wakati mmoja. 

Waandamanaji wa amani wa mwaka 2011 wakaanza kupunguwa, na badala yake Wasyria wengi wakapaswa kuchaguwa baina ya kujisalimisha kwa utawala au kujiunga na makundi ya waasi yaliyoanza kidogo kidogo kugeukia siasa kali za kidini.

Wakati nikiwa nimeshughulika kumlea mwanangu na kufanya kazi mjini Berlin, miaka ikawa nayo inakwenda na hivyo pia machungu na mateso - hata kwa Wasyria waliofanikiwa kukimbia janga na kukimbilia mataifa jirani. Walijikuta wakiwa wamesimama mbele mbele ya maisha yaliyo matupu ambayo yaligeuka kuwa harakati za daima kupapia maisha kwenye jamii ambazo hazikuwapa usalama wowote wa maisha.

Wengine wakapoteza akili, wengine wakafariki dunia kimya kimya au wakamezwa na Bahari ya Mediterenia, na wengine wakafika Ulaya ama Marekani. Wengine wameamua kuendelea kupambana dhidi ya utawala wa kidikteta mjini Damascus kwa kumfungulia mashitaka Assad na jamaa na washirika wake na kuwabebesha dhima ya uhalifu walioutenda. 

Lazima Assad awajibishwe

Mimi ni mmoja ya Wasyria waliopata bahati ya kuishi mbali na vita. Lakini bado matukio ya miaka hii 10 yananiandama. Miaka 10 baada ya kuzaliwa kwa njozi ya heshima na uhuru, habari kutoka na kuhusu Syria bado zingali zinaogofya: mara kundi la wakimbizi wa Syria waanzisha timu ya soka ya watu waliopoteza viungo vyao kwenye vita.

Baadhi ya Wasyria waonesha utundu kwa kutengeneza na kujenga upya mahema yao kila baada ya upepo mkali kwisha. Rais wa Syria apendekeza vituo vya televisheni kutoonesha vipindi vya mapishi ili kutokuwaudhi watu ambao hawana hana mkate.

Nikiwa nimekaa nyumbani kwangu na kusoma yote haya na kuhusu akinamama wa Syria wanaokufa njaa ili waweze kuwapa watoto wao chakula kiduchu wakipatacho, sijui ikiwa nina haki ya kujuta ama kutokujuta. Je, yale maandishi kwenye nguo ya Waad al-Kateab katika Tuzo za Oscars ni sawa na ushauri wa Marie Antoinette "waache wale keki"? 

Sijuwi. Ninachojuwa ni kwamba Syria ni gofu tupu na hakuna njia ya kurejea mwaka 2011. Lakini kupitia maridhiano, kuna njia ya kutoka, na ni haki tu ndiyo inayoweza kuwasaidia Wasyria kuridhiana na kuponya majeraha ya miaka 10 hii iliyopita. Juhudi za Wasyria walioko Ulaya na Marekani kumwajibisha Assad, familia yake na mtandao wa washirika wao kwa uhalifu walioutenda ni hatua za awali.