1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magaidi hawastahili kupewa nafasi duniani

14 Novemba 2015

Dalili zinaashiria wauaji waliofanya mashambulizi ya Paris ni waislamu wenye misimamo mikali ya kidini. Mwandishi wetu Bernd Riegert anasema ni wasaa wa ulimwengu uliostaarabika kutafuta mkakati wa kuukabili ugaidi.

https://p.dw.com/p/1H5sS
Frankreich Terror in Paris Stade de France
Picha: Imago/ZUMA Press

Ufaransa imeshambuliwa. Ulimwengu umeshutuka. Lengo la magaidi hao waoga sio tu kuwalenga wahanga wao kiholela, bali kutulenga sisi. Binaadamu wote, kama Rais wa Marekani Barack Obama alivyosema.

Tunaweza tu kukodoa macho kutizama, tukiwa tumepigwa na butwaa na tukiwa tumejawa na ghadhabu, jinsi magaidi wanavyoweza kufanya mashambulizi katika eneo moja na kuua kiholela bila huruma. Ufaransa, Ulaya na ulimwengu mzima sasa lazima uwe kama kitu kimoja na kuchukua hatua. Waisilamu wenye misimamo mikali, wahalifu wanaotumia nguvu lazima wakabiliwe kutumia mbinu zote zinazowezekana.

Watu waliohusika na mauaji haya ya kutisha, wawe wako nchini Syria, Iraq au mahala pengine popote pale, lazima wapatikane na kuangamizwa haraka iwezekanavyo.

Kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, halijatangaza vita dhidi ya Ufaransa; limetangaza vita dhidi ya watu wote walio huru. Kwa kutilia maanani maadili ya Ufaransa - uhuru, usawa na udugu - ulimwengu sharti uchukue msimamo dhidi ya ugaidi. Fursa muhimu ya kufanya hivi ingekuwa kesho Jumapili wakati mataifa 20 tajiri yatakapokusanyika mjini Antalya nchini Uturuki kwa mkutano wa kilele. Majeshi ya Marekani, Urusi na pengine ya jumuiya ya kujihami ya NATO kutoka Ulaya sharti yaungane pamoja dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq. Na hili linahitaji kufanyika haraka iwezekanyavyo.

Riegert Bernd Kommentarbild App
Mwandishi wa DW, Bernd Riegert

Baada ya mashambulizi ya Charlie Hebdo mwezi Januari mwaka huu, wanasiasa wa mataifa mbalimbali waliandamana pamoja kuonyesha mshikamano. Ilikuwa ishara nzuri, lakini haitoshi tena. Wauaji hao wasio na huruma pengine wanaelewa tu lugha ya mauaji na machafuko.

Usajili wa watu wanaoweza kuwa wauaji miongoni mwa vijana wa Ulaya umepuuzwa kwa muda mrefu mno. Jitihada za kuwageuza kuwa na misimamo mikali lazima zizuiwe kwa nguvu zote. Kama raia wa Ulaya watasafiri kwenda Syria au Iraq kwa mafunzo na wapiganaji wa jihadi, basi angalau safari zao kurejea Ulaya lazima zizuiwe kwa vyovyote vile.

Inaweza kumtokea mtu yeyote

Mizozo yote kati ya mataifa sasa inatakiwa kuwekwa pembeni kwa sababu mtu yeyote anaweza kuwa muhanga mwingine. Siku ya Ijumaa kulitolewa pia onyo la kutokea shambulizi la kigaidi nchini Urusi. Uturuki imeshambuliwa na magaidi mwezi Oktoba. Mji wa Madrid nchini Uhispania ulishambuliwa mwaka 2004 na jiji la London nalo likashambuliwa mwaka 2005.

Hakuna ajuae ni kundi lipi la magaidi Ulaya au Marekani linalosubiri kumuangamiza. Ama kwa upande wa Rais wa Syria Bashar al Assad, jumuiya ya kimataifa inaweza kupata tumbo joto kwa sababu yake mara tu nguvu za kundi la Dola la Kiislamu IS zitakapovunjwa kabisa.

Mbali na mzozo wa wakimbizi unaoikabili Ulaya, sasa pia tuna mzozo wa ugaidi, pamoja na kitisho kisichotarajiwa. Sasa Ulaya inatakiwa idhihirishe kama kweli inaweza kusimama pamoja na kushirikiana. Usalama wa wakazi wote unahatarishwa. Kuishi kwa amani kuko hatarini. Jawabu la viongozi wa kisiasa Ulaya, Marekani na Urusi sasa lazima liwe: Tutajilinda wenyewe!

Mwandishi:Bernd Riegert

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri:Caro Robi