1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Kwa nini tumuamini Trump?

Mohammed Khelef
6 Februari 2019

Kwa nini tulemazwe na kijembe kuhusu umoja wa kitaifa kilichomo kwenye hotuba ya Donald Trump? Ndivyo anavyouliza Michael Knigge, ambaye kwenye maoni yake anaeleza Trump si muumini wa umoja wa Wamarekani.

https://p.dw.com/p/3CoAN
USA Ansprache zur Lage der Union in Washington
Picha: picture-alliance/AP Photo/The New York Times/D. Mills

Kama zilivyokuwa hotuba zake mbili za awali kabla ya kikao cha Congress, Rais Trump alichagua jana kubakia kwenye hotuba iliyoandikwa. Na matokeo yake, rais huyu wa Marekani akatoa kile kinachoweza kuelezwa kama hotuba ya kawaida ya kijadi kwa taifa, badala ya mporomoko wa maneno yake ya kuchapiachapia, ambayo kawaida ndiyo yanayozitambulisha hotuba zake.

Kwenye hotuba yake ya kwanza mbele ya baraza la Congress lililogawika, Trump hakumtukana wala kumdhihaki yeyote, hakutishia kuiangamiza nchi yoyote ya kigeni, hakutangaza hali ya dharura ya usalama ili aweze kujenga ukuta wake kwenye mpaka wa Mexico.

Kwa hakika, hata zile kaulimbiu zake za kampeni: "Ifanye Marekani Iwe Tukufu Tena" na "Marekani Kwanza" hakuzitaja hata mara moja.

Deutsche Welle Englisch Michael Knigge
Michael Knigge, DW Washington.Picha: DW

Badala yake, kwa kiini chake, hotuba ya Trump ilikuwa na wito mmoja tu lakini ulio mrefu: kuushinda mgawanyiko wa kivyama kwa maslahi ya umoja wa kitaifa.

Hapana shaka, hapo katikati ilikuwa ikiingiliwa na maneno ya hapa na pale dhidi ya wahamiaji haramu, kuishambulia Iran, washirika wanaonuka wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO aliojitapa kwamba atawalazimisha walipe. 

Kuumaliza mkwamo

Trump alilitolea wito baraza la Congress kuuvunja mkwamo wa kisiasa, kuunganisha tafauti za kale, kutibu majeraha, na kuwa na moyo wa mapatano na mashirikiano. Tukiwa pamoja tu, Trump aliiambia Congress, ndipo Marekani itaweza kukomesha migawanyiko inayoichanachana vipande vipande. Tukiwa wamoja tu, ndipo tunaweza kuyatatua matatizo ya mjuda mrefu yanawaandamana mamilioni ya Wamarekani kama vile uwezo wa kupata huduma za afya au ajira za kugharamia maisha.

Na unajuwa nini? Trump yuko sahihi. Yuko sahihi kwamba ushirikiano na muafaka tu ndivyo viwezavyo kuishinda migawanyiko ya kisiasa ya taifa lake. Yuko sahihi kwamba masuluhisho ya kudumu kwa matatizo kama vile miundombinu iliyochakaa, huduma za afya za gharama kubwa na zisizopatikana, mfumo wa uhamiaji na mengine mengi yanaweza tu kutatuka kupitia hatua za pamoja na maridhiano.

Mgawanyaji mkuu

Tatizo ni kwamba, kama rikodi zake zioneshavyo, Trump ni mtu wa mwisho kabisa kuwa na hamu na uwezo wa kufikia maridhiano ya kweli. Ikiwa kuna chochote ambacho dunia imejifunza kwake kwenye kipindi hiki cha miaka miwili akiwa madarakani, ni kwamba muafaka wa kweli na ushirikiano nje ya mipaka ya kivyama ni mambo yasiyofikirika kichwani mwa Trump.

Kwa hakika hasa, amefanya mengi ya kuligawa taifa kuliko mtangulizi wake yeyote.

Mwandishi: Michael Knigge
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Daniel Gakuba