1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Mahakama ya Kimataifa ya Rwanda ilijitahidi

Amina Mjahid
8 Novemba 2019

Mahakama ya Kimataifa ya Rwanda iliyaorodhesha mauaji na ubakaji kama uhalifu wa mauaji ya kimbari na kuweka mfano duniani na ndio maana mahakama hiyo inapaswa kuthaminiwa, anasema Fred Muvunyi.

https://p.dw.com/p/3Si4E
25 Jahre Internationaler Strafgerichtshof für Ruanda
Picha: Getty Images/AFP/A. Joe

Mji wa Arusha kaskazini mwa Tanzania ndio mwenyeji wa mahakama hiyo ndogo ambayo imesikiliza mambo maovu yaliYofanywa wakati wa mauaji ya kimbari na kutoa uamuzi wa kushtukiza katika historia ya maamuzi duniani. 

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kuhusu Rwanda (ICTR) iliyoundwa na Umoja wa Mataifa miaka 25 iliyopita, imeshatoa hukumu kadhaa kwa waliopanga mauaji hayo. Nchini Rwanda kabila la Watutsi walilengwa na kujaribu kuangamizwa kabisa.

Pia Wahutu, ambao hawakuwa na misimamo mikali na kutofuata amri ya kuua au kuwasaliti majirani zao, nao waliuwawa na zaidi ya Wanyarwanda milioni 1 waliangamia kwa siku 100.

Mwandishi wa maoni haya mwenyewe anasimulia jinsi shangazi yake alivyouwawa pamoja na watoto wake katika mauaji hayo. La kushangaza ni kwamba aliyewatendea unyama huo alikuwa mume wa shangazi yake anayetokea kabila la Wahutu, ambaye alifanya mauaji hayo baada ya kushawishika kuwa mkewe na wanawe hao walikuwa na damu ya Kitutsi.

Hii yote ikitokana na baadhi ya vyombo vya habari wakati huo vilivyoeneza chuki na uwongo. 

Fred Muvunyi wa Idhaa ya Kiingereza kwa ajili ya Afrika ya DW
Fred Muvunyi wa Idhaa ya Kiingereza kwa ajili ya Afrika ya DWPicha: DW/F. Görner

Wanyarwanda waliuwawa bila huruma, sehemu ya miili yao kukatwa katwa na kuzikwa, huku wanamgambo wakianza kula nyama na kunywa damu ya binaadamu. Wanawake wa Kitutsi walibakwa. 

Mahakama ya Kimataifa ya Rwanda ilisikiliza mambo yote haya, na kuwashitaki watu 93, wakiwemo wanasiasa, wafanyabiashara, wanajeshi, maafisa wa serikali, waandishi habari na viongozi wa kidini.

Kesi zote 80 zilikamilika na kuwa mahakama ya kwanza kutambua ubakaji kama njia ya kuwaadhibu wahalifu wa mauaji ya kimbari. 

Mauaji hayo yalikuwa mabaya na ya kuogofya lakini kwa bahati mbaya hayaonekani kutoa mafunzo kwa jumuia ya kimataifa au kwa wahalifu kote duniani. Katika jimbo la Darfur nchini Sudan watu 300,000 waliuwawa lakini bado waliohusika na mauaji hayo hawajashitakiwa. 

Takriban watu 400,000 wameuwawa tangu maandamano ya kutaka mageuzi yalipoanza nchini Syria, mwaka 2011 yaliosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kando na hayo maelfu kwa maelfu ya Wayemen pia wameuwawa tangu mwaka 2015.

Nchini Cameroon nako watu takriban 300 wameuwawa katika maeneo ya watu wanaozungumza Kingereza. Mashirika yakutetea haki za binaadamu pamoja na wataalamu wanakiona kile kinachotokea Cameroon kama mwanzo wa mauaji sawa na yale yaliotokea Rwanda. 

Ni wakati muafaka sasa ambako dunia inahitaji mfumo wa kimataifa wa kutoa haki ili kuwaadhibu wahalifu duniani. 

Kwa wale wanaoona mahakama za ndani na kitaifa kama njia mbadala ya kuwaadhifu wahalifu, hana imani na mahakama kama hizo akisema kwa kawaida huwa zinaendeshwa na watu wale wale walio na damu mikononi mwao na uhuru wa kuendesha kesi katika mahakama hizo ni wa kutiliwa shaka huku idadi ya waathiriwa wa uhalifu ikipanda.

Kitu kitakachosaidia ni mahakama za kimataifa.