1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Marekani, Ulaya haziko pamoja dhidi ya Urusi

6 Juni 2014

Viongozi wa G7 wamemalizia mkutano wao, huku Marekani na Ulaya zikitarajia kuimarisha msimamo wao wa pamoja juu ya mgogoro wa Ukraine, lakini ushirikiano huo unakabiliwa na changamoto kubwa.

https://p.dw.com/p/1CDZS
Christoph Hasselbach wa Deutsche Welle
Christoph Hasselbach wa Deutsche WellePicha: DW/P. Henriksen

Mjini Brussels, Kansela Angela Merkel aliusifu ushirikiano miongoni mwa mataifa saba yaliyoendelea kwa viwanda duniani kuelekea mzozo wa Ukraine hadi sasa. Lakini ushirikiano huu hivi punde utaporomoka.

Kuna mgawanyiko wa kidiplomasia kati ya Ulaya na Marekani. Mipasuko pia iko wazi ndani ya Ulaya huku mataifa yaliyokuwa kambi ya Mashariki yakihofia kuwa kiraranga mwengine makuchani mwa mwewe Putin. Alipokuwa ziarani Poland, Rais Barack Obama wa Marekani alisimamia upande wa nchi hizo na kuziahidi ulinzi.

Watu wengi mashariki mwa Ulaya wanawashuku majirani zao wa Magharibi kwa kuweka mbele mafungamano yao ya kibiashara na Urusi kuliko usalama wao. Ambapo Wamerakani wanatuma wanajeshi mashariki, Wafaransa wanapanga kuwauzia Warusi meli za kivita, huku Washington ikitoa wito wa vikwazo vikali zaidi, kansela wa zamani wa Ujerumani anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa na Rais Vladimir Putin wa Urusi.

Hofu za Mashariki

Watu kwenye mataifa kama vile Poland, Estonia na Latvia wanajiuliza ni nani wamtegemee pindi mambo yakenda kombo. Kijembe kama kilivyo, uhalali wa Putin kuikalia Crimea akidai kuwasaidia raia wanaozungumza Kirusi kwenye mkoa huo, kinaweza pia kutumia kwenye eneo zima la Baltic. Na angalau kwa sasa Jumuiya ya Kujihami ya NATO haijapanga kuzuia kuvamiwa kwa nchi kama vile Estonia, kwa mfano.

Hata kama mtazamo huu si lazima uwe ni wa kila mmoja, lakini lazima uzingatiwe kwenye muktadha wa ushirikiano huu, kwani pengo linazidi kuwa kubwa hasa linapokuja suala la vikwazo. Kiwango cha tatu cha vikwazo, ambacho kwa hakika kina nguvu na kinaweza kuiathiri sekta nzima ya uchumi, bado hakijatekelezwa.

Na kama uamuzi huo unawategemea Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Rais Francoise Hollande wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, basi kamwe vikwazo hivyo havitakuwapo.

Obama mkali, Ulaya baridi

Obama ameonesha msimamo mkali zaidi. Hata hivyo, ni rahisi zaidi kwake kufanya hivyo, maana wakati Ulaya ya Magharibi inaingiza kiwango kikubwa cha nishati kutoka Urusi, Marekani inategemea zaidi soko la nishati la Urusi.

Swali linalozunguka sasa mjini Brussels ni ipi itakuwa hali kwenye duru ya tatu ya vikwazo. Hakuna jawabu ya moja kwa moja iliyotolewa hadi sasa. Uvamizi wa Urusi mashariki mwa Ukraine unatakiwa kuwa sababu inayotosha kuchukua uamuzi huo, lakini hakutakuwa na chengine cha ziada kutafsiri hapo.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na mataifa hayo saba yenye utajiri wa viwanda, vikwazo zaidi vitaamuliwa ikiwa tu Urusi itaendelea kuizorotesha hali ya mashariki mwa Ukraine. Lakini hili linaweza kutafsiriwa kwa njia nyingi tafauti.

Merkel anasema hakupaswi kuwepo na uwekaji wa moja kwa moja wa vikwazo vya ziada, badala yake wanachama wa kundi la mataifa hayo saba sharti kwanza wakubaliane kabla ya hatua kama hizo kuchukuliwa. Hili linaifanya milango mengine michache kuwa wazi.

Mwandishi: Christoph Hasselbach
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo