1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni : Mauaji ya halaiki Rwanda - Kushindwa kwa Jumuiya ya Kimataifa

7 Aprili 2014

Jambo hilo lisingelipaswa kutokea: Mauaji ya halaiki mbele ya macho ya ulimwengu! Hata watoto wachanga na vikongwe waliuwawa. Wanamgambo waliteketeza hata nyumba za ibada ambapo watu walikuwa wamejihifadhi.

https://p.dw.com/p/1Bd7Q
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili (DW) Andrea Schmidt.
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili (DW) Andrea Schmidt.Picha: DW

Katika kipindi cha siku 100 serikali ya wakati huo na wanamgambo wake waliwauwa zaidi ya watu 800,000. Hususan walioandamwa walikuwa ni watu wa jamii ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani ambao walikuwa wamejaribu kuwasaidia majirani na marafiki zao.

Lakini suala ni kwa nini hakuna mtu aliechukuwa hatua licha ya kutolewa kwa tahadhari na mapema?Takriban miezi mitatu kabla ya kuzuka kwa mauaji hayo,mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa(UNAMIR) nchini Rwanda Romeo Dallaire alituma ujumbe kwa wakuu wake walioko New York ambapo alionya katika kile kinachojulikana kama "Fax ya Mauaji ya Halaiki " yenye kufafanuwa mipango ambapo kwayo wanamgambo wakiwa kwenye makundi ya kuanzia watu 40 wanaweza kuuwa zaidi ya watu 1,000 katika kipindi kisichozidi dakika 20.

Wakati mauaji hayo yalipokuwa yamepamba moto,Dallaire alituma tena ujumbe wa dharura kwa Umoja wa Mataifa wa kuisihi itume wanajeshi zaidi wa kulinda amani na kuwapa mamlaka thabiti ya kulinda wananchi.Badala yake Umoja wa Mataifa ukaanza hata kupunguza vikosi vyake vilioko nchini humo yumkini kutokana na hofu ya kuja kukabiliana na balaa la kushindwa kama lile lililowakuta wakati ilipoingilia kati nchini Somalia na wakayafumbia macho mauaji hayo na kukataa kukiri juu ya ouvu huo uliokuwa ukitokea.

Wakati huo huo Ufaransa iliendelea kuipelekea silaha serikali ya nchi hiyo hadi mwezi wa Juni yaani badala ya kuchukuwa hatua ya kuingilia kati kijeshi kwa "Operesheni ya Turquoise(Takwaz)" ili kuwalinda raia,jeshi la Ufaransa liliwachilia wanamgambo waliohusika na mauaji ya halaiki kuondoka na silaha zao na kukimbilia Congo iliokuwa ikijulikana kama Zaire wakati huo.

Wajibu mpya wa kulinda wananchi

Hususan Umoja wa Mataifa ulikuwa umefedheheka kwa kushindwa kutimiza wajibu wake.Lakini wamejifunza nini kutokana na hilo?Kutokana na kuboronga huko Rwanda,Umoja wa Mataifa na juhudi zake za Kuwajibika kutowa Ulinzi hapo mwaka 2005 umebuni mfumo mpya ambapo mataifa yanawajibishwa kulinda wananchi wake dhidi ya ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, mauaji ya halaiki na kuangamiza jamii.Iwapo nchi inashindwa kutimiza wajibu huo wa kutowa ulinzi jumuiya ya kimataifa inaweza kutimiza wajibu huo na kuingilia kati kijeshi.

Lakini msimamo wa uadilifu pekee hautoshi.Umoja wa Mataifa haukuzuwiya mauaji ya raia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sri Lanka .Hata hivi sasa kuna maeneo ya vita ambayo ni changamoto kwa jumuiya ya kimataifa kuthibitisha kile ilichojifunza kutokana na Rwanda.Kwa mfano maangamizi ya jamii yanayofanyika Jamhuri ya Afrika ya Kati au hali ya machafuko nchini Sudan Kusini.

Lakini kwa nini shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa bado zinakosa mamlaka thabiti ya kutekeleza majukumu yake?Changamoto ni pamoja na umuhimu wa kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mapema kama vile matumizi ya nguvu kupita kiasi.Kuweka viashiria kabla ya hali kuwa mbaya,wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wawe wamepatiwa mafunzo vizuri, kupatiwa silaha na kuwa tayari kukabiliana na hali hiyo kwa ufanisi na uwajibikaji.

Congo ni mfano

Kikosi cha Umoja wa Mataifa kilioko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kinaweza kutumiwa kama mfano wa mambo yote kwa matatizo na njia zinazoweza kutumika kwa ufumbuzi katika shughuli za kulinda amani.Kwa miaka mingi kikosi hicho kimekuwa kikishutumiwa kwa ukosefu wake wa ufanisi na moja kwa moja kuchukiwa na wananchi wa nchi hiyo.Kutokana na kutokuwa na mamlaka thabiti ya kutekeleza majukumu yake mara nyingi hujifanya hawaoni wakati watu wanapouwawa na wanawake kubakwa. Hata hivyo hapo mwaka 2013 kutokana na kuwepo kwa kikosi kipya cha kuingilia kati haraka cha wanajeshi kutoka Afrika chenye mamlaka mpya hali hiyo imebadilika.

Hususan shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa hazipaswi kushindwa kutokana na ukosefu wa fedha na rasilmali.Jumuiya ya Kimataifa lazima ijitolee kwa kila hali kutowa msaada kwa haraka na kuwa na ufanisi hususan kulinda haki za binaadamu katika nchi husika.Matumizi mabaya kutokana na sababu za kisiasa au za kiuchumi lazima yaepukwe.

Jumuiya ya Kimataifa hapo mwaka 1994 ilitenda kosa kubwa sana.Lazima isifumbie macho tena uhalifu wa aina hiyo.Mauaji ya halaiki yamegharimu maisha ya watu 800,000 nchini Rwanda. Watu wengine milioni tatu wameuwawa katika vita vya Congo ikiwa ni matokeo ya mauaji hayo ya halaiki.Jambo hilo pia halipaswi kusahauliwa.

Mwandishi: Andrea Schmidt/Mohamed Dahman

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman