1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Mdahalo kati ya Trump na Biden wageuka mechi ya fujo

Daniel Gakuba
30 Septemba 2020

Baada ya mdahalo wa kwanza wa televisheni baina ya Rais Donald Trump na mpinzani wake wa chama cha Democratic Joe Biden usiku wa Jumanne, walioutazama hawayaamini masikio yao. Maoni ya Carla Bleiker (DW Washington).

https://p.dw.com/p/3jDFL
USA Präsidentschaftswahlen TV Debatte Trump Biden
Picha: Jonathan Ernst/Reuters

Kilichotarajiwa kuwa mjadala wa kupingana kwa hoja ili wapiga kura ambao hawajaamua nani kati ya Trump na Biden wamuunge mkono waweze kufanya maamuzi, kimeishia kuwa vurugu mithili ya malumbano ya kifamilia kati ya wajomba wawili, ambapo mmoja amemzidi mwingine kupaza sauti, huku mwenzake akichekacheka kwa kejeli na kutingisha kichwa, akishindwa kumdhibiti mpinzani wake.

Marekani ni nchi inayopita katika migogoro mkubwa kabisa; mripuko mkubwa wa virusi, majanga ya kimazingira yenye uhusiano na mabadiliko ya tabianchi, na pengo linalozidi kupanuka kati ya raia wake weupe na weusi.

Carla Bleiker APP Kommentarbild vorläufig
Carla Bleiker, DW-Washington

Lakini katika mdahalo wa kwanza wa moja kwa moja baina ya wagombea hawa wa vyama vya Republican na Democratic, kumeshuhudiwa Rais ambaye hakumuachia nafasi mpinzani wake ya kukamilisha hata sentensi moja, na hakuwasilisha chochote kutoka upande wake ambacho kinaweza kuisuluhisha migogoro hiyo.

Trump ashindikana kudhibitiwa

Pale kiongozi wa mdahalo, Chris Wallace alipojaribu kumkumbusha Rais Trump, kwamba timu yake iliafiki kuwa kila mgombea atapata fursa ya kuzungumza kwa dakika mbili bila kukatizwa, na Trump akaridhia kumwachia nafasi Biden aendelee, alichomudu kukitamka Biden ni kwamba Trump huwa haheshimu ahadi zake.

Lakini kwa sehemu kubwa ni Donald Trump aliyeuvuruga mdahalo huo kiasi kwamba aliyeuongoza ameshindwa kumdhibiti, na ilikuwa inaumiza kichwa kuutazama.

Joe Biden alikuwa na mapungufu yake pia. Amemwita Trump kikaragosi, mwenendo ambao haufai kwenye jukwaa la kisiasa. Na kuhusu swali juu ya nani anaweza kupiga kura kwa njia ya posta, wapi na kwa muda gani, Biden ameboronga kama kawaida yake, na jibu lake halikuwa na mbele wala nyuma.

Kuna haja gani ya mdahalo, kama hakuna hoja

Trump aliyetia fora katika kuutia aibu mdahalo wa kirais, na mwendeshaji wa mdahalo huo alishindwa kabisa kumrudisha katika njia sahihi. Hata Biden hakuwa na sauti ya kumzuia Trump, isipokuwa tu pale alipozungumzia utumishi wa mtoto wake Beau jeshini nchini Irak, na Trump akataka kulikwepa hilo na kujaribu badala yake kumuingiza mtoto mwingine wa Biden, Hunter, akimhusisha na tuhuma za ufisadi.

Kama hakuna mdahalo kwa sababu mgombea mmoja hawezi kumuacha mwingine azungumze, hakuna haja ya kuwepo mdahalo. Kinachofuata kwenye kalenda, ni mdahalo kati ya Makamu rais wa sasa Mike Pence, na mgombea mwenza wa Joe Biden, Kamala Harris.

Baada ya hapo itafuata midahalo mingine miwili kati ya Trump na Biden. Ikiwa Joe Biden angeamua kuisusia midahalo hiyo mingine, hilo linaweza kueleweka baada ya kiloja cha jana, lakini anaweza kuonekana kama muoga aliyesalimu amri.

 

Carla Bleiker (DW Washington)