1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ulaya yaisaidia Ugiriki ili iisaidie tena

Mohammed Khelef20 Agosti 2015

Licha ya bunge la Ujerumani kupitisha awamu ya tatu ya mkopo kwa Ugiriki lakini wabunge wanajuwa huu hautakuwa mkopo wa mwisho kwa taifa hilo linalodidimia vibaya kiuchumi, anaandika Sabine Kinkartz.

https://p.dw.com/p/1GI8U
Kura ya uamuzi bungeni kuisaidia tena Ugiriki kwa awamu ya tatu ya mkopo.
Kura ya uamuzi bungeni kuisaidia tena Ugiriki kwa awamu ya tatu ya mkopo.Picha: Reuters/A. Schmidt

Je, unaikumbuka filamu iitwayo "Groundhog Day"? Katika filamu hiyo ya miaka ya '90, mtabiri wa hali ya hewa mwenye kiburi anajikuta akikutana na siku ile ile tena na tena, pakiwa hapaonekani njia ya yoyote ya wakati kubadilika. Hili linahusianaje na deni la Ugiriki? Kwa mengi.

Mkopo huu wa mwisho ulioidhinishwa na Bundestag hapo jana hautaiondoa Ugiriki kimiujiza kutoka kwenye dimbwi la madeni yake. Utaiimarisha tu hali ilivyo sasa. Inawezekana muelekeo wa jambo lenyewe ni tafauti kidogo, kwa kuwa mara hii wakopeshaji wanajaribu kubadili sera za Ugiriki, lakini hilo halilitatui tatizo la msingi.

Kati ya euro bilioni 86 ambazo Ugiriki itapokea, bilioni 54 zitakwenda kwenye kulipia deni lililopo kwa wakopeshaji hawa hawa wanaotoa hizi fedha. Hii inaunda mduara wa papo kwa papo wa deni jipya ili kulipa la zamani. Na deni hilo jipya nalo pia lazima lije lilipwe. Lakini kwa fedha zipi?

Na Sabine Kinkartz
Sabine KinkartzPicha: DW/S. Eichberg

Benki za Ugiriki zitapewa euro bilioni 25 zaidi kuzizuwia kufilisika kwa mara nyengine tena. Kiwango kidogo cha fedha kitaingia kwenye bajeti ya serikali, lakini kiuhalisia tayari kiwango hicho kimeshatumika. Ugiriki tayari ina mengi ya kuyalipia na mara tu pesa inapoingia, hutoka. Sasa inakuwaje?

Mkopo kwa mageuzi

Mkopo huu wa tatu umejifunga kwenye mageuzi ya kiserikali, kiuchumi na kijamii nchini Ugiriki. Nchi hii inahitaji mamlaka madhubuti ya kifedha, na fursa za ukwepaji kodi kukatwa kabisa. Serikali inapaswa kupambana na ufisadi na uchumi usio rasmi na kuunda mtandao wa usalama wa kijamii.

Haya yote yanaonekana kuwa mazuri, lakini swali ni ikiwa je fedha walizopewa zinatosha kulisimamisha wima taifa lililokwishaporomoka kabisa kabisa? Au fedha nyengine zaidi zitahitajika? Kwa kasi gani mageuzi haya yanaweza kutekelezwa? Hapana shaka, si kwa siku moja.

Kilicho wazi ni kuwa lau mambo yatakwenda hivi hivi, mkopo wa mara ya nne utafuatia, na kisha wa tano, na wa sita, na hivyo hivyo kuendelea. Na hilo ndilo linaloturejesha kwenye ile filamu ya "Groundhog Day". Mtabiri wa hali ya hewa mwenye kiburi anagundua njia ya kubadili wakati kwa kufanya mabadiliko.

Ni hicho ndicho ambacho wakopeshaji wa Ugiriki wanapaswa kukifanya, wakijuwa kuwa kamwe hawatazipata pesa zao kwa mtindo huu wa kulifunika deni kongwe kwa jipya. Wanapaswa kuukiri ukweli huu na kukabiliana na matokeo yake.

Mwandishi: Sabine Kinkartz/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Daniel Gakuba