1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya kashfa ya Kanisa Katoliki Ujerumani

Abdu Said Mtullya10 Januari 2013

Wahariri wanatoa maoni juu kashfa inayohusu uchunguzi wa unyanyasaji wa kingono katika kanisa katoliki nchini Ujerumani na juu ya matukio ya Ireland ya kaskazini

https://p.dw.com/p/17H4v
Askofu Stephan Ackermann wa Kanisa Katoliki nchini Ujerumani
Askofu Stephan Ackermann wa Kanisa Katoliki nchini UjerumaniPicha: dapd

Kanisa katoliki nchini Ujerumani limeisimamisha kazi ya mtaalamu aliekuwa anafanya uchunguzi juu ya madai ya watoto kufanyiwa ufidhuli na makasisi.Lengo la uchunguzi huo huru lilikuwa kutoa mwanga juu ya kadhia za unyanyasi wa watoto uliofanyika hata kabla ya mwaka wa 1945 katika kanisa katoliki.Maaskofu wa kanisa hilo wamesema hawana imani na mchunguzi huyo na kwamba watamtafuta mwengine! Juu ya uamuzi wa kanisa hilo kumfukuza mchunguzi huyo Christian Pfeiffer gazeti la "Neue Osnabrücker" linauliza ni nani hapa anaeudhuru zaidi wajihi wa kanisa kama siyo maaskofu wenyewe!

Mhariri wa gazeti la" Rheinpfalz" anasema kanisa katoliki nchini Ujerumani linataka jamii iuone ukweli kwa macho ya kanisa hilo.Mhariri huyo anasema ni kweli kwamba kanisa katoliki limeyashughulikia madai juu ya unyanyasi uliofanywa na makasisi kwa watoto, na limechukua hatua kwa waliohusika.Lakini kukuru kakara za sasa kuhusiana na mchunguzi aliefukuzwa zinakaikaribi picha ya jamii juu ya kanisa linaloitaka jamii hiyo ioune ukweli kwa kutumia vigezo vya kanisa. Hiyo ni ishara inayoleta madhara makubwa kwa kanisa.

Gazeti la "Thüringischer Landeszeitung" linataka ukweli udhihirike kwa manufaa ya wahanga. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba waliofanyiwa ufidhuli na makasisi bado wanasibika. Majeraha hugeuka makovu, lakini maumivu ya roho hayana mwisho. Waliofanyiwa ufidhuli na makasisi wanayo haki ya kuujua ukweli.Katika kanisa katoliki wapo wale wanaotaka kuufunikiza ukweli.Watu hao asilani wasipewe mwanya wa kufanikiwa.

Ireland ya Kaskazini:

Ghasia zimekuwa zinaendelea kwa siku kadhaa ,nchini Ireland ya Kaskazini zilizosababishwa na mvutano baina ya wanaotetea bendera ya Malkia "Union Jack" na wale wanaopinga.Mhariri wa gazeti la "Sächsiche" anasema sababu ya ghasia hizo ni ya kipuuzi lakini athari zake ni kubwa sana. Wapinzani wa kutundikwa bendera ya Uingereza,"Unioni Jack," kwenye manispaa ya mji wa Belfast, wanakereka roho na ndiyo sababu wamechochea ghasia.

Yanayotukia sasa yanakumbusha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Irelanda ya Kaskazini vilivyochukua muda wa miaka zaidi ya 30 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 3000. Mzozo juu ya bendera unaonyesha jinsi hali ilivyoendelea kuwa nyeti katika Ireland ya Kaskazini. Ghasia hizo zinatoa ishara mbaya kwa wawekaji vitega uchumi, hasa wakati huu ambapo Ireland ya Kaskazini inajitahidi kuleta ustawi wa uchumi. Vijana wanaoleta ghasia wanapaswa kutambua kwamba wanajiharibia mustakabal wao.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Yusuf Saumu