1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jee ni sahihi kupiga marufuku mavazi?

16 Agosti 2016

Wahariri wanatoa maoni juu ya juhudi za kidiplomasia za Waziri Steinmeier za kuutatua mgogoro wa Syria. Na pia wanasema mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump hataweza kubadilika.

https://p.dw.com/p/1Jj1Z
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: picture-alliance/AP Photo/C. Owen

Mhariri wa "Der Tagesspiegel" anasema katika juhudi za kuutatua mgogoro wa Syria Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier za kuutatua mogoro wa Syria amekutana na Waziri mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov.

Mawaziri hao wamejaribu kutafuta njia za kuwasaidia watu wa Aleppo, mji wa kaskazini mwa Syria uliozingirwa na majeshi ya serikali.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linatilia maanani kwamba wakati Waziri Steinmeier amependekeza wazo la kuanzisha njia ya angani ili kupeleka mahitaji kwa ndege, wakati Urusi imesema mapigano yatasimamishwa kwa muda wa siku tatu ili kuruhusu misaada kuwafikia watu katika mji huo wa Aleppo.

Juu ya hali hiyo mhariri wa gazeti la "Der Tagesspiegel" anasema kuzungumkuti kinaendelea kuhusu mgogoro wa nchini Syria.

Naye mhariri wa gazeti la "Badische Tagblatt" anasema hali ya mji wa Aleppo ni ya mkanganyiko, na bila shaka Waziri Steinmeier aliyajua hayo kabla ya kuenda Urusi. Mhariri huyo anaeleza kuwa wenye usemi katika mji wa Aleppo ni makundi yenye itikadi kali pamoja na serikali ya Assad. Ndiyo sababu mtu anaweza kutuhumu kwamba ziara ya Waziri Steinmeier nchini Urusi ilikuwa na malengo mengine.

Mji wa Aleppo hatimaye utaingia katika mikono ya serikali ya Assad kutokana na msaada wa Urusi. Mhariri anaziambia nchi za magharibi kuwa zitapaswa kuzungumza na Urusi juu ya mustakabal wa Syria.

Jee ni sawa kupiga marufuku vazi la Burka


Mjadala juu ya kulipiga marufuku vazi la Burka, linalofunika uso wote, umezuka nchini Ujerumani. Mhariri wa "Kölner -Stadt Anzeiger" anasema ni kweli kwamba vazi hilo ni ishara ya kupinga maridhiano,na kujitenga na jamii. Lakini siyo sahihi kulipiga marufuku.Mhariri huyo anaeleza kwamba sheria ya kupiga marufuku haitafanya kazi katika maeneo ambako uhuru unapaswa kulindwa.

Wanawake waliojifunika nyuso
Wanawake waliojifunika nyusoPicha: picture-alliance/dpa/B. Roessler

Naye mhariri wa "Main Post" anasema kila mtu anao uhuru wa kujiamulia mambo yake, mradi hajiingizi katika uhuru wa mtu mwengine.Jamii huru inahitaji stahamala. Gazeti la "Die Welt" linasema mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump hatabadilika.

Mhariri wa gazeti hilo anasema nyota ya Trump inaendelea kufifia.Anaeleza kwamba kwa miezi kadhaa waendeshaji kampeni yake wamekuwa wanatumai kuona mabadiliko. Hata hivyo sasa imethibiti kuwa wazi kabisa kwamba Trump hatabadilika.

Chama cha Republican kimo katika hatari ya kuchakazwa vibaya katika uchaguzi. Ndiyo sababu chama hicho sasa kinatafakari mkakati wa kuelekeza nguvu katika kunusurika, badala ya kuweka kipaumbele katika kampeni ya uchaguzi.

Lakini mhariri wa "Die Welt" anauliza jee wafuasi wa Trump watakubaliana na mkakati huo?

Mwandishi:Mtullya Abdu.

Mhariri: Gakuba Daniel