1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Josephat Charo21 Mei 2007

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wamejishughulisha na kazi ya jeshi la Ujerumani nchini Afghanistan na mabadiliko ya uongozi katika kampuni ya Siemens.

https://p.dw.com/p/CHSv

Gazeti la Ostsee la mjini Rostock limesema vita nchini Afghanistan sasa vimeliathiri jeshi la Ujerumani. Hujuma ya siri dhidi ya wanajeshi wa Ujerumani wakati walipokuwa wakinunua vitu katika soko la Chaiferoshi mjini Kundus, limedhihirisha wazi dhihiri shahiri vipi juhudi za kisiasa nchini humo zinavyoonekana kuwa kama hatua ya kujidanganya.

Ujerumani sio sehemu ya makundi yayopigana nchini Afghanistan, wanajeshi wake wanalinda juhudi za kuijenga upya nchi hiyo katika eneo lililo salama na tulivu la kaskazini. Na wanamgambo wa Taliban wanafahamu fika swala hilo kiasi cha kuweza kutofautisha, lakini ukweli wa mambo unaonekana kuwa tofauti kabisa kuliko inavyofikiriwa.

Wakati wa msimu wa mapukutiko bunge la Ujerumani, Bundestag, liliidhinisha kurefushwa kwa muda wa wanajeshi wa Ujerumani kuendelea kubakia Afghanistan. haikuwa rahisi kuupisha uamuzi huo hususan ikizingatiwa hatari kubwa inayozidi kuwakabili wanajeshi wa Ujerumani walio nchini humo.

Mhariri wa gazeti la Ostsee akimalizia hoja yake anasema hakuna chaguo lengine la kuubadili uamuzi wa kutuma jeshi la Ujerumani kwenda Afghanistan kwani kuondoka kutasababisha waasi wa Taliban wajiimarishe.

Nalo gazeti la Westfälische Rundschau la mjini Dortmund limesisitiza kuwa ni watu wachache mjini Berlin wanaozungumzia mawazo ya Wajerumani katika sehemu mbalimbali humu nchini. ´Ni kitu gani tulichopoteza nchini Afghanistan, tafia lililosahaulika na Mungu?´ ameuliza mhariri wa gazeti la Westfälische Rundschau.

Bila shaka jambo la busara ni kujiuliza wanachokitaka Waafghanistan. Je wanataka taifa la kiislamu lililo na mifumo ya kizamani ya haki na elimu chini ya utawala wa mashehe au kambi kubwa za mafunzo ya kigaidi katika nchi jirani zenye uwezo wa kinyuklia za Pakistan na Iran? Nchi hizi ndizo zinazofaa kuchukua nafasi ya majeshi ya mataifa ya magharibi nchini Afghanistan ambayo yameikalia kwa muda mrefu, yametumia fedha nyingi na kupata hasara kubwa.

Mada nyengine inahusu mabadiliko ya uongozi katika kampuni ya Siemens. Majina yaliopendekezwa yalitajwa sana katika vyombo vya habari wiki iliyopita, lakini jina la Peter Löscher anayetakiwa aiokoe kampuni ya Siemens halikuwa katika orodha hiyo. Mhariri wa gazeti la Financial Times Deutschland amesema uteuzi wa bwana Löscher ni wa kushangaza. Hata hivyo watu wanasubiri kuona ikiwa uteuzi huo utazaa matunda.

Swali muhimu linaloulizwa ni je kiongozi huyo mpya analazimika kufanya nini na ataleta mabadiliko gani katika kampuni ya Siemens? Kampuni hiyo inakabiliwa na kashfa ya ufisadi iliyoitumbukiza katika mzozo mkubwa wa kutoaminiwa tena. Peter Löscher kama kiongozi mpya anatakiwa atoe maelezo ya kulainisha mambo lakini wakati huo huo awe mpatanishi wa ndani na nje ya kampuni hiyo.

Mhariri wa gazeti la Westfalen Blatt kutoka Bielefeld kwa maoni yake anasema mtu hatakiwi kuitwa Löscher, ndio aweze kuzima moto unaowaka katika kampuni ya Siemens. Na pia si lazima mtu awe meneja wa kampuni ya kutengeneza dawa ili aweze kuwa na ujuzi wa kidaktari kutibu magonjwa. Hadhi ya kiongozi mpya wa Siemens iko katika kiwango kingine kabisa. Löscher au mzima moto wa mjini Munich yuko katika nafasi nzuri ya kuikoa kampuni ya Siemens ingawa anakabiliwa na kibarua kigumu.