1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Josephat Charo12 Desemba 2007

Rais Putin anapania kubakia madarakani

https://p.dw.com/p/CabI
Rais Vladimir Putin (kulia) na naibu wa kwanza wa waziri mkuu, Dmitry MedvedevPicha: AP

Baada ya rais Vladamir Putin wa Urusi kumtaja naibu waziri mkuu Dmitri Medvedev kama mrithi wake, Medvedev anatarajiwa kumtaja rais Putin kuwa waziri mkuu.

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo katika maoni yao wanaiona hiyo kuwa njama kubwa ya rais Putin kutaka kuendelea kubakia madarakani.

Gazeti la Tageszeitung la mjini Berlin linasema mambo mengi yanajitokeza baada ya kutajwa Dmitir Medvedev kuchukua nafasi ya rais Putin. Hatua hiyo inaonekana kuwa mojawapo ya juhudi za kuhakikisha rais Putin anabakia madarakani.

Kitu kimoja kilichojitokeza wazi hivis asa ni kwamba baada ya uchaguzi utakaofanyika mwezi Machi mwaka ujao Urusi itakuwa na rais mpya atakayehakikisha kuendelezwa kwa sera za rais Vladamir Putin. Kwa hiyo matumaini ya mageuzi ya sera za ndani na za kigeni hayapo.

Idadi kubwa ya warusi na pia wanasiasa wa nchi za magharibi huenda waridhishwe na ukweli huu, kwa kuwa jambo la muhimu sana ni uthabiti wa Urusi. Lakini gharama yake ni demokrasia kukandamizwa.

Gazeti la Pforzheimer Zeitung limeeleza wazi kwamba rais Putin ataendelea kubakia kiongozi mwenye mamlaka makubwa katika siasa za Urusi wakati atakapochukua wadhifa wa waziri mkuu.

Mhariri amesema rais Putin atafaulu kufanya hivyo kwa kumtumia mrithi wake, Dimtri Medvedev, ikizingatiwa kuwa kiongozi huyo hatarajiwi kuleta mabadiliko yoyote ya kisiasa.

Rais Putin amefaulu katika miaka iliyopita kupata utiifu wa viongozi wote wa ikulu ya Kremlin wanamtii. Sasa anatarajiwa kuchukua wadhifa wa waziri mkuu lakini anaweza kutumia uwezo wake kumpa maagizo rais mtarajiwa Dmtri Medvedev. Demokrasia ya kweli iliyotarajiwa na upinzani nchini Urusi sasa haitarajiwi kupatikana.

Gazeti la Esslinger Zeitung linasema rais Vladamir Putin ambaye bado ni kiongozi katika ikulu ya Kremlin alipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge huku chaka chake cha United Russia kikipata wingi wa thuluthi mbili ya kura zote zilizopigwa, kama ilivyotakikana.

Mhariri anasema kama iliyopangwa rais Putin anatakiwa abakie kiongozi mwenye mamlaka makubwa katika siasa za Urusi. Ikiwa rais Putin ataendelea kujihusisha sana katika siasa au pengine kuwa kiongozi wa baadaye wa kampuni ya Gazprom, ni jambo litakalokuwa na umuhimu mkubwa. La msingi ni kwamba mfumo mzima wa rais Putin utaendelea kuwepo bila mabadiliko yoyote. Medvedev atakuwa mtiifu kwa rais Putin na kibaraka wake.

Gazeti la Landeszeitung linakisia lengo la rais Vladamir Putin. Mharari anasema kutumia hatua ya kumchagua Medvedev, rais Putin anataka kuhakikisha wizani sawa kati ya wasomi wa ikulu ya Kremlin mjini Moscow, ili kuiwezesha Urusi kuwa dola lenye ushawishi mkubwa wa kisiasa duniani. Enzi ya rais Putin kwa hiyo bado haijamalizika, kwa sababu mfumo mzima wa Putini unabakia.

Lakini ikiwa yeye atabakia kuwa kiongozi mwenye mamlaka makubwa nchini Urusi, ni jambo ambalo linaweza kuchukua mkondo wowote.

Mhariri wa gazeti la Landeszeitung anauliza, ´Je timu ya kiongozi mwenye mamlaka makubwa aliye katika ofisi isiyo na mamlaka makubwa nchini na kiongozi mdhaifu aliye katika ofisi yenye mamlaka makubwa nchini itaweza kufanya kazi? Je idara ya ujasusi itawatii mahakimu wa mjini Petersburg?´

Mhariri anamalizia kwa kusema nchi za magharibi zitajua zinakabiliwa na dola la aina gani ikiwa Urusi itakuwa thabiti.