1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani

Charo, Josephat4 Agosti 2008

Kiongozi wa chama cha Verdi asafiri bure kwa ndege ya Lufthansa na China yafungia tovuti

https://p.dw.com/p/EqDq

Katika maoni yao hii leo wahariri wa magezeti ya Ujerumani wanazungumzia tiketi ya bure aliyopewa kiongozi wa chama cha wafanyakazi cha Verdi hapa Ujerumani, bwana Frank Bsirke, na kampuni ya ndege ya Lufthansa kuendea likizoni nchini Marekani na hatua ya China kuzuia tovuti katika mtandao wa internet huku michezo ya Olimpiki ikikaribia kuanza Ijumaa wiki hii mjini Beijing.

Gazeti la Nordwest Zeitung linaikosoa China kwa kuzuia tovuti katika mtandao wa mawasiliano wa internet. Kwanza kabisa mhariri wa gazeti hilo amekasirishwa sana kwamba kamati ya kimataifa ya Olimpiki, OIC, haitaki wala haiwezi kuchukua hatua yoyote dhidi ya uamuzi huo wa China. Viongozi wa kamati ya OIC wamekuwa kama vikaragosi vya utawala wa China.

China inavunja ahadi ilizotoa wakati wa michezo ya Olimpiki na sasa kamati ya kimataifa ya Olimpiki inabakia ikiikosoa China tu kwa uoga huku ikiwa haina meno yoyote ya kukabiliana nayo. Mhariai anasema hali hii kiurahisi inahatarisha ufanisi wa michezo ya mjini Beijing.

Mhariri wa gazeti la Nordwest Zeitung anatabiri kwamba hapatakuwa na hisia za kuwepo uhuru, uwazi na maelewano kati ya watu wa nchi mbalimbali katika michezo ya Olimpiki ya mwaka huu mjini Beijing. Ukweli huu utakumbusha hali ilivyokuwa wakati michezo hiyo ilipofanyika mjini Moscow nchini Urusi mnamo mwaka wa 1980 na mjini Seoul nchini Korea Kusini mnamo mwaka wa 1988.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung linasema mwenendo wa China kutumia mfumo wa ukandamizaji hakuna awezaye kukosa kuufahamu, ikiwa pia ni pamoja na maafisa wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki. China ni nchi ambayo uchumi wake unakua kwa haraka katika karne hii ya 21. Medali zitazoshindwa na wanamichezo wa China katika michezo ya Beijing zitatoa ishara ya ukakamavu wan China ndani na nje ya nchi.

Gazeti linasema Wachina bila shaka watafurahia ushindi wao, lakini ukweli kwamba China inazuia uhuru wa vyombo vya habai haupaswi kupuuzwa. Mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine anasisitiza kuwa marufuku ni marufuku.

Gazeti la Süddeutschezeitung limetoa maoni kuhusu tiketi ya bure ya ndege aliyopewa kiongozi wa chama cha wafanyakazi cha Verdi hapa Ujerumani, bwana Frank Bsirke, na kampuni ya ndege ya Lufthansa aliyotumia kwenda likizoni mjini Los Angeles Marekani siku chache kabla mgomo wa wafanyakazi wa Lufthansa kuanza.

Je bwana Bsirke alikuwa mjanja kwa kukubali tiketi hiyo ya bure? Mhariri anasema haukuwa uamuzi wa busara kukubali safari hiyo kwani inaonekana kama njama ya kampuni ya Lufthansa kumbembeleza alegeze msimamo wake kuhusu mishara ya wanachama wa chama cha wafanyakazi cha Verdi wanaofanyakazi na kampuni hiyo. Mtu mwenye uzoefu kama Bsirke anatakiwa kulifahamu hilo. Yeye ni mtu huru, lakini inaonekana hajafahamu kikamilifu uhuru una maana gani kwake kuhusiana na swala hili.

Je bwana Bsirke anatakiwa ajiuzulu? Linauliza gazeti la Berliner Zeitung na kujibu; la hasha!

Hatimaye bwana Bsirke amefaulu kupata matokeo mazuri katika wakati ambapo vyama vya wafanyakazi vinapoteza wanachama wake na ushawishi. Kwa miaka kadhaa bwana Bsirke ameonekana kuwa muendeshaji mapambano ya kitabaka na ndio maana baraza la utawala la Lufthansa halikumuondoa. Kwa hiyo kiongozi huyo anatakiwa akumbuke mwendo mrefu wa kwenda kwao huko Ostsee. Gazeti linakisia pengine wakati mwingine bwana Bsirke atasafiri katika daraja la pili la treni kwenda kwao badala ya kusafiria daraja la kwanza katika ndege ya Lufthansa.