1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 40 tokea Armstrong atue mwezini.

Abdu Said Mtullya20 Julai 2009

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya maadhimisho ya mwaka wa 40 tokea binadamu atembee mwezini.

https://p.dw.com/p/It4K
Miaka 40 iliyopita Neil Armstrong alikuwa mwanadamu wa kwanza kutua na kutembea mwezini.Picha: AP


Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya maadhimisho ya mwaka wa 40 tokea binadamu atue mwezini , na juu ya mvutano baina ya Marekani na Israel kuhusiana na ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi.


Leo umetimu mwaka wa 40 tokea mwanadamu atue na atembee katika mwezi.Mhariri wa gazeti la Trierischer Volksfreund anasema hatua hiyo, miaka 40 iiyopita, ilikuwa ya kihistoria. Anasema tukio hilo liliwapa wamarekani hisia za matumaini na kuwarudishia moyo wa fahari .Hatahivyo, mhariri wa gazeti la Trierischer Volksfreund anasema fahari hiyo ilitoweka haraka sana . Baada ya kuonekana kwamba Marekani iliishinda Urusi katika mashindano ya kudhibiti anga za mbali.Wanaanga wengine 10 waliokuwamo katika chombo cha Apollo waliofuata nyayo za Armstrong , leo hawashangaliwi sana.

Mhariri anasema yumkini hayo yanatokana na ukosefu wa ari ya ujasiri wa miaka 40 iliyopita. Mharirri huyo anaeleza kuwa filamu zinazotengenezwa Hollywood juu ya vita vya anga za mbali zinawaburudisha na kuwaliwaza watu kiasi kwamba hatua kubwa iliyochukuliwa na Armstrong miaka 40 iliyopita inaonekana kuwa ni kiduchu cha pembeni tu.

Gazeti la Fränkischer Tag linazungumzia juu ya maadhimisho ya mwaka wa 40 tokea Armstrong atue mwezini kwa kuzingatia mazingira yaliyofuatia kumalizika kwa vita baridi.Gazeti hilo linasema ni jambo zuri , kwamba leo pana ushirikiano wa kimataifa katika utafiti wa anga za mbali. Leo limekuwa jambo la kawaida kuwaona watu wa mataifa mbalimbali kwenye stesheni ya anga ya kimataifa.

Katika maoni yake leo, gazeti la Badische linazungumzia juu ya mvutano baina ya Isreal na utawala wa Obama kuhusu ujenzi wa makaazi ya walowezi ya kiyahudi.

Utawala wa Obama unaitaka Israel isimamishe ujenzi wa makao zaidi ya walowezi wa kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina. Lakini serikali ya Isreal inapinga hayo. Juu ya msimamo huo wa Israel, gazeti la Badische Zeitung linasema serikali ya Israel inapaswa kujua kwamba msimamo huo hautakosa kuwa na madhara.

Israel inapaswa kutambua kwamba mtazamo wa rais Obama juu ya Mashariki ya kati ni wa dhati na hakika msimamo huo ndio utakaomfanya awe msuluhishi wa kweli katika mgogoro wa Mashariki ya Kati baina ya Wapalestina na Waisraeli.

Mhariri wa gazeti la Badische Zeitung anasema kutokana na msimamo wake wa dhati, labda rais Obama atafanikiwa, pale ambapo wengine waliojaribu walishindwa, yaani kuleta amani katika Mashariki ya kati.


Mwandishi/ Mtullya.

Source/Deutsche Zeitungen.