1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAONI YA WAHARIRI

Abdu Said Mtullya3 Agosti 2011

Wabunge wa Marekani wafikia mwafaka dakika za mwisho

https://p.dw.com/p/129jm
Rais Obama na Spika wa Bunge John Boehner baada ya nwafaka kufikiwa.Picha: picture alliance/dpa

Marekani na duniani kote watu wametoa pumzi ya faraja baada ya mapatano kufikiwa juu ya kuukabii mgogoro wa deni wa nchi hiyo.

Wahariri wa magazeti ya hapa nchini wanatoa maoni yao juu ya mapatano hayo.

Gazeti la Hannoversche Allgemeine linasema angalau mapatano ya kwanza yamefikiwa juu ya kuutatua mgogoro wa madeni wa Marekani. Mhariri wa gazeti hilo anaeeleza kuwa hayo ndiyo mtu anayoweza kuyasema juu ya mwafaka uliofikiwa jana na wabunge wa Marekani.

Lakini mhariri wa gazeti la Neue Presse anasema mvutano uliokuwapo juu ya njia ya kuutatua mgogoro wa bajeti wa Marekani umeonyesha udhaifu wa Rais Obama. Mhariri huyo anaeleza kuwa Wabunge fulani wenye itikadi kali walimteka nyara Rais Obama, kwa kutumia lugha ya tamathali. Mhariri wa gazeti hilo anasema hao ni watu wanaofuata nadharia ya mwanasayansi Charles Darwin, "juu ya mwenye nguvu ndiye anaendelea kuishi." Rais Obama anawategemea watu hao. Jambo hilo linamfanya awe dhaifu kiasi cha kuyateketeza matumaini ambayo watu walikuwa nayo juu yake hapo awali.

Mhariri wa gazeti la Schwäbische Zeitung pia anasema mgogoro wa madeni wa Marekani umeonyesha udhaifu wa Rais Obama. Mhariri huyo anaeleza kwamba kauli mbiu ya Obama, "Yes We Can, ndiyo tunaweza, sasa imegeuka ,No We can't ,hapana hatuwezi".! Jee kimetokea nini kwa mwanasiasa huyo mwenye haiba yenye mvuto, alieahidi kuleta mabadiliko katika Ikulu ya Marekani.
Mhariri wa Berliner Zeitung anasema balaa la Merekani kushindwa kulipa madeni yake limeepushwa lakini anauliza jee nchi hiyo imesimama wapi?

Anaeleza kuwa mwafaka uliofikiwa haujakibadilisha kiwango kisichopimika cha madeni ya Marekani. Kisiasa Marekani imegawanyika. Nchi hiyo imetingwa na tatizo la ukosefu wa ajira,wakati inafikia ustawi wa uchumi wa kiwango cha chini. Maalfu ya askari wake wanapigana vita vilivyoshindikana nchini Afghanistan. Uzito wa Marekani katika masuala ya kimataifa umepungua na kufikia kiwango cha chini kisichokuwa na mtihili. Ni urari wa kusikitisha kwa dola hilo kuu.

Mhariri wa Stuttgarter Zeitung anazungumzia juu ya maafa yaliyotokea Lampedusa nchini Italia. Wakimbizi 25 walikutwa wamekufa katika mashua ambayo haikufaa kufanyia safari!

Mhariri huyo anasema ule utayarifu tu wa watu hao kusafiri katika chombo hohe hahe na kustahabu hatari kubwa, unaonyesha jinsi walivyobanwa na shida. Hao ni watu kutoka Somalia, Eritrea, wanaokimbia makwao kwa sababu ya njaa na udhalimu wa kisiasa. Na jee Ulaya inafanya nini? Hakuna anawashughulikia watu hao. Kulinganisha na idadi ya wakimbizi wanaohudumiwa na Kenya ,wakimbizi wanaokuja Ulaya ni kama tone tu la mvua baharini ,lakini Ulaya inajifanya haiwaoni watu hao.!

Mwandishi/Mtullya abdu/ Deutsche Zeitungen/

Mhariri/-Abdul-Rahman