1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wazungumzia ziara ya Kansela Merkel nchini Israel

Mtullya, Abdu Said19 Machi 2008

Katika maoni yao leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya ziara ya kansela Merkel wa Ujerumani nchini Israel.

https://p.dw.com/p/DRDW
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na waziri mkuu wa Israel Ehud OlmertPicha: AP


Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamesema katika maoni yao kuwa ziara ya Kansela Angela Merkel pamoja na hotuba yake zimeimarisha hali ya kuaminiana baina ya  Israel na Ujerumani.

Hatahivyo baadhi ya wahariri wamesema katika hotuba yake Kansela Merkel angeliweza pia kuzungumzia masuala ambayo si ya kupendeza sana kwa Israel.

Juu ya ziara hiyo mhariri wa gazeti la RHEIN-NECKER anaesifu uhusiano baina ya Ujerumani na Israel ameeleza kuwa kwa kuzingatia historia ya nchi mbili hizo  uhusiano huo wa ndani na wa kirafiki ni kama muujiza.

Ziara ya kihistoria ya Kansela Merkel nchini Israel imeimarisha hali ya kuaminiana baina ya waisraeli na wajerumani.

Mhariri huyo ametilia maanani  kuwa Kansela Merkel amefuata nyayo za Kansela wa kwanza wa Ujerumani baada ya vita kuu kumalizika, Konrad Adenauer, ambae pamoja na mwanzilishi wa taifa la Israel  Ben Gurion waliweka msingi wa  mwanzo mpya katika uhusiano baina ya nchi zao.

Gazeti la BERLINER ZEITUNG linasema ziara ya Kansela Merkel iliyofanyika miaka  zaidi ya 60 baada ya maangamizi ya wayahudi barani Ulaya, haiwezi kuzingitiwa hasa , kama hatua ya kuufanya uhusiano baina ya Israel na Ujerumani uwe wa kawaida.Mhariri wa gazeti hilo anatathmini  ziara hiyo kuwa ni ukurasa mpya katika historia ya watu wa  nchi mbili hizo.

Lakini mhariri wa gazeti la LANDESZEITUNG anasema uhusiano baina ya Israel na Ujerumani ungekuwa wa dhati na maalum  iwapo pia ungelipewa mtihani kwa kuzungumzia hata masuala ambayo  si ya kufurahisha.

Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani katika maoni yake kuwa Kansela Merkel ametumia kauli ya uwazi kabisa kuwalaani  Hamas na Iran kwa siasa zao kali dhidi ya  Israel.

Lakini  gazeti  linasema  Kansela Merkel pia angeliweza kutumia kauli ya uwazi kuitaka  Israel iache kabisa  kujenga makao mapya ya walowezi wa kiyahudi katika maeneo ya wapalestina.

Gazeti la NEUES DEUTSCHLAND linalalamika kwamba kansela Merkel ,wala hakuwa na wasaa wa kuyatembelea  maeneo ya wapalestina achilia mbali  ukweli kwamba  katika hotuba yake kiongozi huyo wa Ujerumani, hakutamka  neno hata moja juu ya wajibu wa Israel katika mgogoro wa  mashariki ya kati.