1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Mtullya, Abdu Said17 Juni 2008

Pamoja na masuala mengine wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya mustakabal wa Umoja wa Ulaya baada ya kura ya maoni nchini Ireland.

https://p.dw.com/p/ELbF
Magazeti ya Ujerumani yazungumzia juu ya uamuzi wa Saudi Arabia kuongeza uzalishaji mafuta.Picha: AP

Magazeti ya Ujerumani  leo yanazungumzia juu ya mustakabali wa Ulaya, baada ya wananchi wa Ireland kuupinga mkataba wa Lisbon katika kura ya maoni.  

Magazeti hayo pia yanatoa maoni  juu ya uamuzi wa Saudi Arabia kuongeza uzalishaji mafuta  kwa kiasi cha lita zaidi ya  milioni 31 kwa  siku.Jee  kimetokea nini kwa  wasaudia?

Tatizo la  ulevi wa kupindukia  miongoni mwa vijana wa Ujerumani pia linazingatiwa  na  wahariri katika safu zao za maoni.

Kuhusu mustakabal  wa  Umoja  wa Ulaya  baada ya kura  ya maoni  nchini Ireland, gazeti la Westdeutsche  Zeitung linauliza jee mradi  wa watu  milioni mia tano  uanguke kwa  sababu  ya  kura za wachache?

Lakini mhariri  wa  gazeti hilo anatilia maanani kwamba swali hilo linaulizwa hasa  na wale  wanaofahamu fika kwamba  mradi huo yaani  mkataba  wa Lisbon  ni uzuri  wa  mkakasi! Kilichomo ndani  ni kipande  cha mti. Gazeti linaeleza kuwa watu wa Ireland wameupinga  mkataba  huo  kwa sababu   hawakuelewa, maudhui  yake- yumkini   hayo  ni  kweli,  lakini wananchi  hao  wanapambana  na  hali halisi  ya kila siku inayotokana  na maamuzi  yanayopitishwa  na viongozi wa Umoja wa Ulaya.

Na gazeti  la  Braunschweiger Zeitung linaongeza  kwa  kusema  kuwa matokeo ya kura ya maoni nchini  Ireland ni ishara ya onyo.

Mhariri  wa gazeti hilo anaeleza kuwa uamuzi  watu  wa  Ireland  kuupinga mkataba wa Lisbon maana yake, ni kuwa serikali  za  nchi  za Umoja wa Ulaya zinapaswa  kutekeleza  siasa zitakazokuwa karibu na wananchi  wao.

Na gazeti  la Döbelner Anzeiger linasema, watu  barani Ulaya  wanataka, ajira,usalama wa  kijamii, uhuru zaidi mipakani, na  bei  zilizotengemaa.


Mhariri  wa  gazeti  la Bild  Zeitung ameshangazwa  na  uamuzi  wa  Saudi Arabia  juu  ya  kuongeza  uzalishaji mafuta.

Wasaudia  wamesema  wataongeza  lita milioni 31 na laki nane kila siku  ili kujaribu kuteremsha bei ya mafuta duniani. Mhariri wa gazeti hilo anauliza jee kimetokea nini? Mhariri anakumbusha  nasaha za aliekuwa waziri wa  uchumi wa  Ujerumani mnamo miaka  ya  60 aliyesema kuwa ,mtu lazima  kwanza amlishe  ng'ombe kabla  ya  kumkamua maziwa. Kila mwuuza duka anajua kwamba anapaswa  kuwahudumia  vizuri  wateja wake ili warudi  tena.

Gazeti linauliza  jee ,Saudi Arabia itapata faidi gani ikiwa bei ya mafuta itaendelea kuwa  kubwa  na  kulazimisha  watu wauze magari yao?

Maoni ya gazeti  la Nordwest Zeitung yanahusu ulevi wa  kupindukia miongoni mwa  vijana  nchini Ujerumani.


Gazeti linatilia maanani kuwa mnamo kipindi cha miaka mitano idadi  ya vijana wanaopelekwa  hospitilani  kutokana  na tatizo la ulevi wa  kutopewa-imeongezeka  mara mbili.

Gazeti linasema, tofauti  na bei ya mafuta  ,bei ya pombe ni ya  chini nchini Ujerumani.

Kutokana na hayo itakuwa  vigumu kuwalinda vijana. Kwani sheria  peke yake haitoshi.