1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini

Mtullya, Abdu Said6 Agosti 2008

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani walalamika kuwa fedha nyingi zinatumika kwa ajili ya silaha badala ya kusaidia juhudi za kupambana na maradhi.

https://p.dw.com/p/ErUT
Mkutano juu ya ukimwi waendelea nchini Mexico.

Katika maoni yao wahariri wamagazeti ya  Ujerumani leo  wanazungumzia juu ya  

mabilioni ya fedha  zinazotumika kwa ajili ya silaha wakati  ni kiasi kidogo tu kinatumika kwa ajili ya  kupiga vita maradhi kama  ukimwi.


Gazeti la Morgenpost linasema yumkini watu wataweza kutoa pumzi ya faraja kutokana na bei ya  mafuta kuanza kupungua.


Magazeti ya Pforzheimer na Wetzlarer Neue Zeitung   yanalalamika juu ya usuhuba unaofanyika kwenye  Umoja wa Ulaya inapohusu kuajiri wafanyakazi.

Juu ya fedha nyingi  zinazotumika kwa ajili ya silaha badala ya kutumia  fedha hizo kwa ajili ya  kupambana  na maradhi gazeti la Braunschweiger linasema kuwa binadamu amepoteza  maadili  ya mshikamano. Ni jambo linalotia uchungu kuona  kuwa miradi mingi inayohusu maradhi ya ukimwi  haiendi sambamba na shabaha za kijamii.

Gazeti  linasema  fedha nyingi sana zinatumika  kwa ajili ya  silaha  duniani wakati  ni kiasi  kidogo tu kinachotolewa kuwasaidia  watu wanaougua  maradhi ya  ukimwi. Gazeti la Braunschweiger linatilia maanani kwamba nchini Uhispania   pameanzishwa  shirika  la misaada  la wasanii   wasiojali  mipaka. Wasanii  hao  wanawatumbuiza pia watoto wenye ukimwi,ili kuwafariji watoto hao.

Mhariri wa gazeti hilo ,anasema litakuwa jambo la  manufaa makubwa ikiwa wasanii  hao watatumbuiza  mbele ya wanasiasa  ili wanasiasa  hao watahayari.


Gazeti la Berliner Morgenpost linasema yumkini  watu wameshakivuka  kipindi kigumu cha  bei ya  mafuta

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa nchi zinazozalisha  mafuta  za shirika la OPEC  hazitapata  manufaa yoyote ikiwa bei ya mafuta  itaendelea kupanda. Kupanda huko kwa bei kunaathiri  ustawi wa uchumi  wa  dunia.

Mhariri wa gazeti la Berliner Morgenpost anatilia  maanani kwamba  hata mwenyekiti wa shirika la OPEC angependelea kuona bei ya mufuta ikiteremka  hadi  kufikia dola 80 kwa pipa moja. Gazeti linasema hayo yanaonesha kuwa dunia  imeshavuka kipindi kigumu katika bei ya mafuta.


Gazeti la Wetzlarer Neue Zeitung linalalamika  kuwa wanasiasa kwenye Umoja wa Ulaya wanaajiri  ndugu zao na  kuwalipa  mishahara  inayotokana na fedha za walipa kodi. Jambo la kushangaza ni kwamba hadi sasa wamekuwa wanaruhusiwa kufanya hiyvo. Lakini sasa baraza la bunge la Umoja  huo linataka kukomesha utaratibu  huo.