1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Adhabu ndogo kwa Aung San Suu Kyi ni ushindi kwa jumuiya ya kimataifa!

Abdu Said Mtullya12 Agosti 2009
https://p.dw.com/p/J8D7
Watu nchini Myanmar wataka San Suu Kyi aachiwe.Picha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya hukumu iliyotolewa kwa kiongozi  wa upinzani nchini Myanmar Aung San Suu  Kyi  na hukumu nyingine iliyotolewa  nchini Ujerumani kwa aliekuwa kamanda katika  jeshi  la Ujerumani wakati wa vita kuu. Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu ya  mkutano mkuu wa chama  cha wapalestina Fatah.

Kama ilivyokuwa inahofiwa na jumuiya   ya kimataifa,  kiongozi wa upinzani  nchini Myanmar San Suu Kyi ameongezewa adhabu na watawala wa kijeshi wa nchi  hiyo.

Jana mahakama  ilimhukumu mwanasiasa huyo kifungo cha miaka  mitatu jela ,lakini adhabu hiyo imebadilishwa, na badala yake ameongezewa miezi 18  ya kifungo cha nyumbani.

Juu ya hukumu hiyo mhariri wa gazeti la Nürnberger Nachrichten anasema jumuiya ya kimataifa  inapaswa  kuitathmini   adhabu hiyo ndogo kuwa ni mafanikio ya kampeni yake. Gazeti hilo linasema sasa  halitakuwa jambo la manufaa kutoa miito juu  ya kuimarisha vikwazo dhidi ya watawala wa Myanmar. Sababu ni kwamba  biashara kati ya nchi  za Umoja  wa Ulaya na Myanmar  ni ndogo sana kiasi  kwamba vikwazo hivyo havitakuwa  shinikizo kwa watawala hao.

Na gazeti la Badische Neueste  Nachrichten linasema hukumu iliyotolewa   kwa San Suu Kyi inaonyesha kwamba utawala wa Myanmar bado upo mbali  sana na demokrasia.

Na nchini  Ujerumani mahakama ya mjini Munic jana ilitoa adhabu  ya kifungo cha maisha  kwa aliekuwa kamanda katika jeshi la mafashisti wa Kijerumani. Mtu huyo Josef Scheungraber-  mwenye  umri  wa miaka  90 alipatikana  na hatia ya kuamrisha mauaji halaiki kwenye kijiji  kimoja  nchini Italia,wakati wa vita kuu.

Juu ya hukumu hiyo gazeti la Allgemeine Zeitung  linasema,  ni muhimu, na pia ni lazima  sana,  kutoa adhabu hiyo, hata kama uhalifu  ulitendwa  miaka 40 iliyopita.

Gazeti hilo linasisitiza kuwa  jambo muhimu ni kwamba haki imetendeka kwa niaba ya wahanga na kwa ndugu na jamaa  wa wahanga  hao.

Gazeti la Sächsiche Zeitung pia linazungumzia juu ya adhabu ya fashisti huyo kwa kueleza kwamba adhabu aliyopewa mtu huyo Scheungraber siyo kashfa, asilani kama anavyodai wakili wake.Gazeti linaeleza kuwa tunachoweza kusema kuwa kashfa ni kwamba hukumu hiyo imetolewa baada ya miaka 40 au 50. Mhariri wa gazeti la Sächsiche Zeitung anasema kuchelewa kutolewa kwa adhabu hiyo kunaonesha ni kwa kiasi  gani , ilikuwa vigumu, baada ya kumalizika vita kuu vya pili , kwa idara za sheria  za  Ujerumani kufuatilia uhalifu uliotendwa  na utawala wa mafashisti.

Gazeti hilo linatahadharisha  kuwa  ,kila mwaka unavyopita ndivyo inavyokuwa vigumu kuthibitisha uhalifu wa mafashisti kwa sababu mashahidi muhimu wameshakufa siku nyingi.

Gazeti la Stuttgarter Zeitung linazungumzia juu ya mkutano mkuu wa chama cha wapalestina, Fatah.

Gazeti hilo linawaambia  wapalestina kuwa sasa umefika wakati wa kuachana  na mkakati  wa kutumia mabavu,kwa sababu makakati  huo  hautafua dafu mbele ya Israel.

Mwandishi/Mtullya Abdu.

Mhariri/Abdul-Rahman