1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri.

Abdu Said Mtullya2 Desemba 2010

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani pia wanazungumzia juu ya mkutano wa jumuiya ya usalama na ushirikiano barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/QOJU
Rais wa Kazakhstan Nursultan Nazarbayev kushoto akimkaribisha Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwenye mkutano wa nchi za OSCE:Picha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani pamoja na masuala mengine leo wanazungumzia juu ya FIFA,mkutano wa kilele juu ya masuala ya usalama, unaomalizika leo, mjini Astana na juu ya mwanzilishi wa tovuti ya wikileaks J Assange.

Kuhusu shirikisho la kandanda Duniani ,FIFA Mhariri wa gazeti la Westdeutsche anasema wakati sasa umefika wa kufanya mageuzi katika muundo wa shirikisho hilo. Mhariri huyo anaeleza kuwa FIFA leo inaamua ni nani atakaepewa jukumu na heshima ya kuwa mwenyeji wa fainali za kombe la dunia za mwaka wa 2018 na mwaka wa 2022.Ni wajumbe 22 watakaotoa uamuzi.Yeyote atakeshinda ni sawa, lakini muhimu la kulitilia maanani ni kwamba FIFA imepoteza imani duniani. Kinachotakiwa sasa ni kufanya mageuzi, siyo tu ya sura za wajumbe bali ya muundo mzima wa shirika hilo.

Mhariri wa gazeti la Badische pia anasema wajihi wa FIFA umevurugika kutokana na madai ya rushwa.Na kwa hiyo, pana haja ya kufanyika mageuzi. Ndiyo sababu kwamba katika kura itakayopigwa leo na wajumbe wa shirikisho hilo,hapatakuwa na mshindi wa dhati.

Gazeti la Lausitzer Rundschau leo linatoa maoni juu ya mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za jumuiya ya usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE, unaomalizika leo katika mji wa Astana, nchini Kazakhstan.Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba Kansela wa Ujerumani Angela Merkel pia ameshiriki kwenye mkutano huo, ingawa madikteta pia walikuwapo. Mhariri huyo anaeleza kuwa ni vizuri kwamba Kansela wa Ujerumani alishiriki kwenye mkutano huo uliofanyika katika mji wa Astana nchini Kazakhstan.

Bibi Merkel alitumia wasaa wa mkutano huo kusisitiza ulazima wa kuyatekeleza maadili ya haki za binadamu katika nchi za jumuiya ya usalama na ushirikiano barani Ulaya.

Gazeti la General Anzeiger linazungumzia juu ya mkutano wa Cancun unaojadili hatari inayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.Lakini gazeti hilo linasema, kinachotokea kwenye mkutano huo ni mchezo wa kutupiana lawama.

Gazeti la Reutlinger General Anzeiger linatoa maoni juu ya mwanzilishi wa tovuti ya Wikileaks, Assange.Gazeti hilo linasema huyo ni mtu mwenye kipaji cha juu sana lakini pia ni mtu mwenye matatizo ya haiba.Lakini bila ya kujali matatizo yake binafsi, alichokifanya ni changamoto kubwa kwa kile kinachoitwa uwazi, usiokuwa na mipaka.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri:M.Abdul-Rahman