1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

260210 CeBIT Vorschau

Josephat Nyiro Charo1 Machi 2010

Kampuni zinazoshiriki kwenye maonyesho ya CeBIT zimepungua

https://p.dw.com/p/MF5W
CeBIT 2010 Kauli mbiu ulimwengu uliounganishwa na mtandaoPicha: Deutsche Messe Hannover

Maonyesho makubwa ya kimataifa ya teknolojia ya mawasiliano yanaanza leo Jumanne katika mji wa Hannover hapa Ujerumani na yataendelea hadi Jumamosi tarehe 6 wiki hii. Mwaka huu maonyesho hayo kama ilivyokuwa hapo mwaka jana, yamepoteza idadi ya waonyeshaji bidhaa.

Kuanzia hii leo makampuni 4157 kutoka mataifa 68 yataonyesha bidhaa zao katika maonyesho ya mjini Hannover, hiyo ikiwa ni idadi ndogo kabisa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Mwaka uliopita idadi ya kampuni zilizoshiriki kwenye maonyesho ya CeBIT mjini Hannover ilipungua na kufikia takriban 4300 ikilinganishwa na mwaka juzi 2008 ambapo kulikuwa na zaidi ya makampuni 5800 kwenye maonyesho hayo. Kwa hiyo si jambo la kushangaza kwamba maonyesho hayo ya CeBIT yanatafuta mtazamo mpya.

Wageni wachache, kampuni chache zinazoshiriki kwenye maonyesho ya mwaka huu, na hamasa ndogo: Tangu miaka ya hivi karibuni umaarufu wa maonyesho ya kimataifa ya teknolojia ya mawasiliano ya mjini Hannover, CeBIT, umekuwa ukipungua. Mwanzoni mwa karne hii ya 21 wageni 800,000 waliyatembelea maonyesho ya Hannover, lakini mwaka jana idadi hii ilipungua kwa asilimia 50, kwa sababu kwa kila kitengo cha teknolojia ya mawasiliano kina maonyesho yake.

Kitengo cha simu za mkononi hukutana kila mwanzo wa mwaka mjini Barcelona nchini Uhispania. Watengenezaji wa kompyuta na watumiaji wa vifaa vya elektroniki huandaa maonyesho yao huko Las Vegas Marekani. Hufanyika pia maonyesho ya kimataifa ya habari na mawasiliano mjini Berlin hapa Ujerumani.

Licha ya hayo Wolfram Fritsch, mwenyekiti wa kampuni ya maonyesho ya Ujerumani, Deutschen Messe AG, anaamini kwamba maonyesho ya CeBIT mjini Hannover bado yataendelea kubakia kuwa makubwa zaidi ulimwenguni katika sekta ya habari na mawasiliano.

"Nadhani maana ya maonyesho ya CeBIT leo imekuwa kubwa zaidi kuliko hapo awali wakati watu laki nane walipohudhuria maonyesho hayo. Maonyesho ya CeBIT yamekuwa maonyesho makubwa zaidi ya kibiashara katika sekta ya teknolojia ya kompyuta ulimwenguni kote. Na maana hii imeendelea kukua na kupanuka."

CeBIT 2010 Flash-Galerie
Mfanyakazi wa kampuni ya IBM kwenye maonyesho ya CeBIT ya HannoverPicha: picture alliance/dpa

Wakati maonyesho ya Hannover yalipokuwa na umaarufu mkubwa wageni 800,000 walivitembelea vibanda mabalimbali kwenye ukumbi wa maonyesho hayo mjini humo. Kwa wageni waliotaka tu kuwinda zawadi za bure za bidhaa mpya zilizoonyeshwa kwa ajili ya kuzitangaza, hakukuwa na mazungumzo ya maana kati yao na wafanyabiashara. Ndiyo maana mwaka jana wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano wakapewa kipaumbele kikubwa. Lakini sasa kuna mabadiliko; mbali na wataalamu, watumiaji binafsi wa bidhaa wamepewa umuhimu kwa sababu wanategemeana katika teknolojia hii ya mawasiliano.

Achim Berg, mkurugenzi wa kampuni ya kimarekani Microsoft hapa Ujerumani, anauona mkondo huu mpya kuwa mzuri kwa sababu kila mahali kazi na wakati wa mtu kupumzika ni vitu visivyoweza kutenganishwa. Mfano mzuri ni aina mpya ya simu ya mkononi iitwayo Smartphone, ambayo itaingia katika masoko hivi karibuni. Kutumia simu hii mtu anaweza kufungua mtandao wa intaneti kwa maana kwamba intaneti itakuwa ikisafiri kila mahali mtu anapokwenda.

Jürgen Kuri, mhariri mkuu wa jarida la maswala ya kompyuta hapa Ujerumani, anasema, "Mada muhimu kwenye maonyesho haya ya CeBIT zitakuwa bila shaka huduma za intaneti kwenye simu za mkononi kwa watumiaji. Hii ina maana mtandao wa intaneti uweze kupatikana kila mahala na habari ziweze kuwafikia watumiaji kwa wakati unaofaa."

Ingawa idadi ya makampuni yanayoonyesha bidhaa zao kwenye maonyesho ya CeBIT imepungua mwaka huu, kunazo kampuni takriban 300 zinazoshiriki kwa mara ya kwanza, ikiwemo kampuni inayotoa huduma za intaneti ya Google na kampuni ya biashara kwenye mtandao wa intaneti Amazon. Kauli mbiu ya maonyesho ya Hannover mwaka huu ni "Ulimwengu uliounganishwa na mtandao." Maonyesho hayo yatalenga kudhihirisha vipi mipaka kati ya kazi na wakati wa mapumziko, au kati ya huduma za simu na mtandao wa intaneti, inavyopotea polepole.

Mwandishi: Wenkel, Rolf/ZPR/Charo,Josephat

Mhariri: Miraji Othman