1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano upande wa Palestina - uchaguzi nchini Israel

Abdu Mtullya12 Juni 2007

Mapigano yapambamoto baina ya Hamas na Fatah kwenye Ukanda wa Gaza wakati nchini Israel chama cha leba chatafuta kiongozi. Wajumbe wa Misri wanaosuluhisha katika mgogoro wa wapalestina wametoa mwito kwa pande zinazopingana juu ya kujadili mpango mpya wa kusimamisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza wakati ambapo watu wasiopungua 20 wameuawa katika saa 24 zilizopita.

https://p.dw.com/p/CHCm
Ehud Barak
Ehud BarakPicha: AP

Miongoni mwa waliouawa ni katibu Mkuu wa chama cha Fatah katika Gaza kaskazini Jamal Abu al Jedian. Habari zinasema kuwa alipigwa risasi mara 41 akiwa hospitalini amelazwa. Na ndugu yake pia alikutwa ameuawa baada ya muda mfupi.

Watu wengine kadhaa wamejeruhiwa katika mapigano ya saa hizo 24 zilizopita baina ya wafuasi wa Hamas na Fatah. Nyumba ya waziri Mkuu wa Palestina Ismail Haniya pia ilishambuliwa kwa gurunedi lililorushwa kwa roketi. Bwana Haniya pamoja na familia yake hawakudhurika katika shambulio hilo.

Msemaji wa Hamas ameeleza kuwa shambulio hilo lilikuwa jaribio la kumwuua waziri mkuu huyo. Hii ni mara ya tatu kwamba nyumba ya waziri Mkuu Haniya imeshambualiwa katika kipindi cha muda mfupi.

Katika kile kinachoonekana kuwa kushtadi kwa mapigano baina ya wafuasi wa Hamas na Fatah pande mbili hizo zimekuwa zinatumia matovuti ili kutoa miito kwa wanachama wao kwa lengo la kuchochea mauaji.

Hapo awali vyama vya Hamas na Fatah vilikubaliana kwa mara ya saba juu ya kusimamisha mapigano ambayo tayari yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 60.

Wakati huo huo uchaguzi wa kiongozi mpya wa chama cha leba unaendelea nchini Israel ambapo aliekuwa waziri mkuu wa hapo awali bwana Ehud Barak anapambana na bwana Ami Ayalon aliekuwa mkuu wa usalama. Uchaguzi huo ni muhimu sana kwa serikali ya mseto nchini Israel. Uchaguzi wa leo ni raundi ya pili baina ya wanasiasa hao.

Akitoa mwito kuomba kura bwana Barak anaejaribu kuduri tena katika ulingo wa siasa baada ya miaka sita amewataka wapiga kura wamchague mtu anaefaa hasaa katika nyakati hizi za vita.

Lakini mpinzani wake bwana Ayalon amewaambia wapiga kura kuwa wanaotaka kuona mapya katika chama cha Leba wamchague yeye.

Hatahivyo utabiri unaonesha kuwa bwana Barak anaweza kushinda kwa kupata asilimia 46 ya kura . Wanachama zaidi ya laki moja wa chama cha leba wanatarajiwa kushiriki katika kupiga kura itakayoamua juu ya nani atachukua nafasi ya Amir Peretz kiongozi wa sasa wa chama cha leba aliedhoofika kisiasa kufuatia vita vya nchini Lebanon vya mwaka jana.

Bwana Peretz ambae ni waziri wa ulinzi pamoja na waziri mkuu Olmert wamelaumiwa vikali kwa kuongoza vibaya vita hivyo.

AM.