1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapatano ya Biashara

30 Septemba 2008

Mapatano ya biashara kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika yatafikiwa-asema waziri wa biashara wa Kenya.

https://p.dw.com/p/FRkq

Kuhusu ushirikiano wa kibiashara kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya, Kenya ina matumaini kwamba mapatano kati ya pande hizo mbili yatafikiwa.

Kenya inatazamia kuwa mapatano hayo yanayolenga kufungua hatua kwa hatua masoko ya nchi masikini kwa bidhaa za nchi za Umoja wa Ulaya ambayo yamezusha mabishano, yatatiwa saini mwishoe.Hii ni kwa muujibu wa waziri-mdogo wa biashara wa Kenya Bw.Omingo Magara alivyoarifu:

Kenya pamoja na jirani zake inajadiliana mapatano mapya kuchukua mahala pa yale yanayotoa nafuu maalumu na ya muda mrefu kati ya Ulaya na koloni zake za zamani ambayo hivi sasa yanakiuka kanuni za Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO).

Umoja wa Ulaya unafanya mazungumzo sawa na haya na kundi la nchi za Afrika-Karibian na Pacifik (ACP) kwa ufupi ili kufikia mapatano yatayoitwa Economic Partnership Agreements-mapatano ya ushirikiano wa kiuchumi -EPA kwa ufupi.

Haya ni mapatano ambayo wakosoaji wanadai yatadhuru hali za maisha za wakulima wa nchi hizo masikini.

"Mara tutukizitatua tofauti ziliopo .....ingawa siwezi kusema lini, ninaweka matumaini ya maafikiano."-waziri huyo mdogo wa biashara wa kenya aliliambia shirika la habari la Reuters.

Kenya ikiwa ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),imetia saini mapatano ya muda Novemba mwaka jana ili kulinda bidhaa zake tangu za kilimo hata za kiviwanda.

Mapatano ya ushirikiano huo wa kiuchummi na umoja wa Ulaya (EPA) yana shabaha ya kukuza maendeleo-endelevu ya kundi la nchi za ACP-Afrika,Karibean na Pacifik.Pia yanalenga kupunguza umasikini na kuhimiza umoja wa nchi hizo.Lakini wasi wasi juu ya kufungua wazi milango ya masoko ya nchi hizo masikini na nafuu za kibiashara umebaki kuwa kizuwizi kikubwa kinachokwamisha mapatano.

Hadi sasa si zaidi ya nusu ya nchi 80 za kundi la ACP zimetia saini mapatano ya muda huku dola kuu za kundi hilo mfano wa Afrika Kusini, zikihoji kuwa mapatano hayo yaweza kudhuru uchumi wa nchi hizo pamoja na kuzuwia muungano .

Kwa muujibu wa mapatano ya mwisho yatakayofikiwa, nchi masikini zinatarajiwa kufungua pole pole masoko yao kwa bidhaa kutoka nchi za Umoja wa Ulaya katika kipindi cha robo-karne ( miaka 25). Baada ya kupita miaka 15, 80% ya bidhaa zinazosafirishwa ngambo kutoka Umoja wa Ulaya zitaingia soko la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC ) na za Jumuiya ya Uiano wa Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC).

Akihutubia hafla moja mjini Milan, j kuhusu uchumi baina ya Kenya na Itali,Bw.Magara alisisitiza lile wazo la Umoja wa forodha miongoni mwa nchi za Jumuiya ya SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

COMESA -soko la pamoja kati ya nchi za Afrika Mashariki na Kusini -Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ile ya Kusini mwa Afrika (SADC) zinazingatia kuunganisha shughuli zao kwa lengo la kuunda soko kubwa zaidi na kushirikiana pamoja katika miradi ya mindo-mbinu na nishati.

Jumuiya ya Afrika Mashariki tayari ina Umoja wa Forodha -Custom Union-unaofanya kazi .Na Jumuiya ya COMESA inapanga kuanzisha umoja wake hadi ifikapo Desemba mwaka huu.Wanachama 15 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inapanga umoja kama huo kuufikia hapo 2010 na wanachama wake 12 walianzisha Eneo la Biashara Huru hapo August mwaka huu.