1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yazuka upya Libya

Admin.WagnerD29 Desemba 2014

Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya amesema makundi ya itikadi kali za kiislamu yameanza harakati mpya za kuviteka tena vyanzo vya mafuta, baada ya shambulio katika matangi ya kuhifadhia mafuta mashariki mwa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/1EBxH
Rakete trifft Öltank im Osten Libyens
Picha: Reuters/Stringer

Shambulio hilo katika eneo la kaskazini lilisababisha moshi mkubwa mweusi kutanda katika anga ya eneo hilo. Akizungumza kutoka mjini Cairo, Misri Waziri wa Mambo ya Nje Mohamed Dairi, alisema shambulio hilo limefanywa na kundi la wanamgambo wa kiislamu lenye makao yake makuu katika mji wa magharibi wa Misrata na ambalo ni tiifu kwa serikali hasimu ya Tripoli.

Alisema makundi ya Kiislamu yamejiunga katika shambulio hilo, ambalo limelazimisha kufungwa kwa bandari kubwa ya kusafrishia mafuta. Afisa mmoja kutoka shirika la mafuta nchini humo Mohammed al-Hariri alisema Jumamosi iliyopita kuwa mapipa 850,000 ya mafuta yaliangamia kutokana na kuripuka kwa matangi matano ya kuhifadhia.

Mapigano yalizukaa katika maeneo ya karibu na eneo kubwa la kuhifadhia mafuta la Sidra, ambalo kwa hivi sasa lipo katika udhibiti wa kundi la wanamgambo lenye kupinga itikadi kali, lenye ushirika na serikali yenye kutambulika kimataifa ambayo ina makaazi yake katika mji wa mashariki wa Tabruk. Mapema mwezi huu serikali ya Tripoli ilijiapiza kulikomboa eneo la Sidra.

Matangi ya mafuta yakiteketea Mashariki mwa Libya
Matangi ya mafuta yakiteketea Mashariki mwa LibyaPicha: Reuters/Stringer

Kwa mara ya kwanza makombola ya angani yaliripotiwa mjini Misrata, kwa kile kilichoonekana kama majibu yaliyosababishwa na shambulio katika vituo vya mafuta. Ahmed al-Musmari, msemaji wa jeshi linaloongozwa na Tobruk, aliuambia mtandao wa habari wa al-Wasat kwamba shambulizi hilo lilikuwa likilenga ngome zilizokuwa zikilenga kushambuliwa wanajeshi wake.

Maafisa usalama mjini Misrata walisema mashambulizi ya anga yalifanyika karibu na uwanja wa ndege, ambapo kombora moja lilishambulia mita 300 kutoka katika mnara wa kuongozea ndege lakini halikufika katika eneo la lami. Afisa ambae alizungumza kwa msaharti ya kutotaja jina lake kwa kuwa hakuidhinishwa kuzungumza na waandishi, alisema shambulizi hilo limesababisha kusimamishwa kwa safari za ndege za shirika la ndege la Uturuki lakini hata hivyo hakuna maafa yoyote yalioripotiwa.

Mohammed al-Dairi Libyen Außenminister
Waziri wa Mambo ya nje wa Libya Mohamed Al DairiPicha: Getty Images/ASHRAF SHAZLY/AFP

Dairi, waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Tobruk alisema makundi ya wenye itikadi kali za kiislamu, baadhi yakiwa na makubaliano ya muungano na kundi kubwa linalojiitwa Dola la Kiislamu, yameongeza wigo wao nchini Libya, ukiwemo mji mkuu wa taifa hilo.

"Kwa bahati mbaya, tumekuwa na wasiwasi hapa Libya kutokana na ongezeko la wapiganaji wa Dola la Kiislamu kutokana na ongezeko la makundi ya wenye itikadi kali kama unavyojua kundi la Ansar Al Sharia limejiunga kufanya mashambulizi tata dhidi ya maeneo yenye hifadhi ya mafuta".Alisema waziri Dairi

Mazungumzo yanayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa kati ya serikali hasimu nchini humo yamepangwa kufanyika Januari 5. Na mpango maalum wa kuiunga mkono Libya wa Umoja wa Mataifa umelaani vikali mashambulizi ya anga ya Misrata.

Mwandishi:Nyamiti Kayora/AFP,APE
Mhariri:Iddi Ssessanga