1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Steve Scalise atoka kwenye kinyang'anyiro cha Spika wa Bunge

Zainab Aziz
13 Oktoba 2023

Chama cha Republican kimeshindwa kuusuluhisha mgawanyiko ndani ya chama hicho hatua ambayo imesababisha kujiondoa mjumbe Steve Scalise kwenye kinyang'anyiro cha Spika wa Bunge.

https://p.dw.com/p/4XUhc
USA, Washington | Steve Scalise
Picha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Baraza la Wawakilishi la Marekani bado linakabiliwa na mivutano ndani ya chama cha Republican kuhusu nani anayeweza kuchukua nafasi ya Spika wa Bunge.

Mgombea wa chama cha Republican Steve Scalise alijiondoa kwenye kinyang'anyiro usiku wa jana Alhamisi baada ya kushindwa kupata uungwaji mkono wa kutosha kuliongoza Baraza la Wawakilishi la Marekani na hivyo kulitumbukiza bunge katika mgogoro mkubwa.

Kiongozi wa wengi katika Bunge la Marekani Steve Scalise
Kiongozi wa wengi katika Bunge la Marekani Steve ScalisePicha: Branden Camp/ZUMA/picture alliance

Kutokana na mivutano katika chama hicho cha Republican mjumbe Steve Scalise katika tangazo la kushtukiza alisema anajiondoa kwenye orodha ya walioteuliwa kuwania nafasi ya Spika wa Bunge.

Scalise alitoa tamko hilo kwa waandishi wa habari muda mfupi baada ya Baraza la Wawakilishi (GOP) bila ya kutarajiwa lilipowaita washiriki wote kwenye makao makuu ya Bunge la Marekani (Capitol).

Ilikuwa ni siku moja tu baada ya Scalise kushinda kura ya siri japo kwa idadi ndogo ya kura iliyofanyika katika kikao cha faragha cha wawakilishi wa chama cha Republican.

Bunge la Marekani mjini Washington
Bunge la Marekani mjini WashingtonPicha: Anna Moneymaker/Getty Images

Wawakilishi kadhaa wa chama cha Republican walishatangaza kuwa hawana mpango wa kumuunga mkono Scalise. Kwa sasa, wabunge wengi wa chama cha Republican wanasema hawana uhakika wa hatua zikazofuata wanapobaini ni mteule gani anaweza kufikisha idadi ya kura 217 ili kushinda jukumu hilo la Spika wa Bunge.

Wajumbe wahafidhina wenye msimamo mkali ndani ya chama cha Republican wanaomuunga mkono rais wa zamani Donald Trump wamejikita kwenye mapambano ya muda mrefu kwa atakae chukua nafasi ya Kevin McCarthy baada ya kutimuliwa kwake.

Wamesisitiza kuwa kiongozi wa wengi Steve Scalise hakuwa chaguo bora. Mpaka sasa hakuna ratiba mpya ya zoezi la kupiga kura ya kumchagua Spika mpya iliyopangwa.

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump
Rais wa zamani wa Marekani Donald TrumpPicha: BRENDAN MCDERMID/REUTERS

Na maadamu hakuna Spika wa Bunge ina maana kwamba shughuli haziwezi kusonga mbele. Wajumbe hawawezi kupitisha ufadhili wowote au kusonga mbele na mswada wa matumizi ya taifa kabla ya wasiwasi uliopo wa uwezekano wa kufungwa shughuli za serikali ifikapo mwezi ujao.

Vyanzo: AFP/AP