1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kutekeleza vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini

Isaac Gamba
7 Agosti 2017

Rais wa Marekani Donald Trump pamoja na mwenzake wa Korea Kusini Moon Jae-in wameahidi kutekeleza vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini ikiwa ni baada ya azimio la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/2hns3
Trump ermuntert Polizisten zu mehr Gewalt
Picha: Reuters/J. Ernst

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya White House katika mazungumzo yao kwa njia ya simu viongozi hao wawili wamekubaliana kuwa Korea Kaskazini ni kitisho kikubwa na kinachoongezeka kwa Marekani, Korea Kusini, Japan pamoja  namataifa mengine duniani.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa viongozi hao wamekubaliana pia kutekeleza maazimio yote na kutoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kufuata nyayo hizo.

Azimio hilo lililoandaliwa na Marekani linaizuia Korea Kaskazini kuuza nje baadhi ya bidhaa zitokanazo na raslimali zake  kama vile madini aina ya makaa ya mawe, chuma pamoja na samaki na pia linalenga kudhibiti idadi ya wafanyakazi katika mataifa ya nje wanaotoka Korea Kaskazini ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku mikataba mipya ya kibiashara na nchi hiyo.

Azimio hilo lililoungwa mkono bila kupingwa na nchi zote 15 wananchama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likitekelezwa  litaikosesha Korea Kaskazini mapato ya kiasi cha dola bilioni tatu  sawa na euro bilioni 2.7  zitokanazo na mauzo ya nje ya bidhaa kutoka nchini humo.

 

China yaunga mkono vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini

Philippinen Asean-Ministertreffen | Wang Yi
Waziri wa mambo ya nje wa China Wang YiPicha: picture alliance/AP Photo/B. Marquez

Wakati huohuo waziri wa mambo ya nje wa China  Wang Yi amesema hapo jana kuwa vikwazo vipya dhidi ya Korea Kaskazini ambayo imekuwa ikikabiliwa na vikwazo vya Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2006 ndio hatua sahihi ya kuidhibiti nchi hiyo kutokana na majaribio yake ya makombora.

Wang Yi amesema na leo hii kuwa  nchi yake inaunga mkono hatua inayochukuliwa na Korea Kusini katika kukabiliana na mvutano uliopo katika rasi ya Korea  na kuwa China inatarajia kuona nchi hizo mbili za Korea Kusini na Korea Kaskazini zinajadiliana pamoja juu ya kutafuta suluhu ya mvutano huo.

Marekani ilikuwa imetishia kuweka mbinyo kwa china pamoja na kuyawekea vikwazo makampuni ya China yanayofanya biashara pamoja na Korea Kaskazini.

Marekani na china  walianza mazungumzo mapema mwezi Julai baada ya Korea Kaskazini kufanya jaribio lake la kwanza mnamo Julai 4 la kombora la kutoka bara moja kwenda jingine na kufuatia na jaribio lingine la pili la kombora la aina hiyo la Julai 28.

 

Korea Kaskazini kulipiza kisasi

Nordkorea Kim Jong-un
Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong-unPicha: Reuters/KCNA

Wakati huohuo Korea Kaskazini imeapa hii leo kuwa itaimarisha hazina yake ya makombora na kufyatua makombora mengine zaidi kama hatua ya kulipiza kisasi kutokana na Marekani kuunga mkono vikwazo vikali vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa dhidi yake.

Katika taarifa iliyotangazwa na shirika la habari la serikali, Korea Kaskazini imesema vikwazo hivyo vinaashiria ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa taifa hilo ambavyo vimesababishwa na mpango wa Marekani wa kutaka taifa hilo litengwe.

Korea Kaskazini imesema vikwazo hivyo havita ilazimisha nchi hiyo kujadili juu ya mpango wake wake wa nyukilia au kuachana na juhudi zake za kuimarisha shughuli zake za kinyukilia.

Mwandishi: Isaac Gamba/dw/ape

Mhariri: Iddi Ssessanga