1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Kenya kushirikiana kibiashara

Sudi Mnette
7 Februari 2020

Marekani na Kenya zimekubaliana kuanzisha mazungumzo ambayo yatayawezesha mataifa hayo kuwa na mpango wa makubaliano ya kwanza ya pamoja ya kibiashara.

https://p.dw.com/p/3XOnX
USA Uhuru Kenyatta und Donald Trump in Washington
Picha: Imago/R. Sachs

Hatua hiyo inafikiwa katika kipindi hiki ambacho Marekani imegubikwa na wasiwasi wa uwekezaji wa China katika eneo zima la bara la Afrika.  Muda mfupi baada ya mkutano wao uliofanyika katika Ikulu ya Marekani viongozi hao kwa pamoja walitangaza azma yao ya  kuanza mazungumzo rasmi.

Rais Trump alionekana akitoa maelekezo kwa mwakilishi wa wa masuala ya biashara wa Marekani Robert Lighthizer, kutoa taarifa rasmi kwa bunge la nchi hiyo, kuhusu namna mazungumzo hayo yatakavyofanyika. Na wakati huo huo Lighthizer alitoa taarifa yenye kueleza kwamba anaamini makubiliano hayo na Kenya yatasaidia sana katika jitihada za Marekani katika kujiingiza vyema katika bara la Afrika.

Mpango wa kukuza wigo wa ajira wa Kenya

Kenya kama taifa la Afrika Mashariki, lenye uhitaji wa kutanua wigo wa soko lake la nje, nafasi za ajira kwa mamilioni ya vijana sawia na kuimarisha sarafu yake, imekuwa na ongezeko la watalii kutoka Marekani pamoja na makampuni kadhaa kama Alphabet Inc.

Rais Uhuru Kenyattawa taifa hilo aliiambia jumuiya ya wafanyabiashara wa Marekani amedhamiria kukuza hatma ya uchumi wa taifa lake kupitia mpango wa Marekani wa kukuza uchumi wa Afrika wa Marekani unaoitwa. Africa Grouth and Opportunity Act, ambao unatoa nafasi kwa mataifa yaliokusini mwa jangwa la Sahara kusafrisha maelfu ya bidhaa bila ushuru hadi 2025. Rais huyo aliongeza kwa kusema pande zote zimeonesha ari ya kufanikisha makubaliono mapya kwa haraka.

Endapo makubalinao yatafikiwa Kenya inatarajiwa kuwa kitovu cha makampuni ya Kimarekani am,bayo yanafanya biashara zao barani Afrika na nje ya mipaka ya bara hilo. Biashara ya Kenya na Marekani kwa sasa inatajwa kuwa ya kiasi cha dola bilioni 1, ingawa inatabiriwa kuongezeka zaidi. Aidha duru zinaeleza maafisa wa Marekani wanatarajiwa kwenda Kenya Mei, na Kenyatta ana matumaini ya kukamilisha mchakato wa makubaliano na Marekani ndani ya kipindi cha miaka miwili toka sasa.