1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Ufaransa waitisha mkutano kuhusu Haiti

Kabogo Grace Patricia15 Januari 2010

Mbali na kuitishwa kwa mkutano huo wa kimataifa, Marekani imetoa kiasi dola milioni 100 kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Haiti.

https://p.dw.com/p/LWCa
Mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince unavyoonekana sasa ukiwa umeharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea siku ya Jumanne.Picha: AP

Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa wameitisha mkutano wa kimataifa kuhusu Haiti kufuatia nchi hiyo kukumbwa na tetemeko la ardhi siku ya Jumanne.

Rais Sarkozy pia anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais wa Brazil, Lula Inacio da Silva na Waziri Mkuu wa Canada Stephen Harper. Rais huyo wa Ufaransa amesema nchi yake itashirikiana kwa karibu na washirika wake wa Umoja wa Ulaya na pia atafanya ziara Haiti kwa ajili ya kukutana na rais wa nchi hiyo, Rene Preval.

Wakati huo huo, Rais Obama ametangaza kuwa Marekani itatoa msaada wa awali wa dola milioni 100 kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Haiti na kwamba juhudi za uokozi za Marekani zinaendelea kupangwa haraka iwezekanavyo.

Kiasi watu 50,000 wanahofiwa kufa kutokana na tetemeko hilo la ardhi na watu wengine wanaokadiriwa kufikia milioni tatu wanahitaji msaada wa dharura.