1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaadhimisha siku ya uhuru kwa migawiko

Iddi Ssessanga
5 Julai 2020

Waandamanaji wanaorudiarudia maneno ya "Maisha ya Watu Weusi ni Muhimu" wanatupiana maneno na wafuasi wa Trump nje ya Ikulu: Siku ya uhuru wa Marekani iliadhimishwa Jumamosi kwa makabailiano na mgawiko.

https://p.dw.com/p/3eol2
USA, Washington I Donald Trump I Salute to America
Picha: picture-alliance/C. Kleponis

Huku ikipambana kudhibiti virusi vya corona na wakati huo ikikabiliana na wimbi la waandamanaji wanaopinga ubaguzi wa rangi, Marekani imegawika pakubwa, ambapo tofauti hazikuonekana kupungua katika siku ambayo kawaida huadhimisha utaifa na umoja.

Jambo moja watu waliokuwa nje ya ikulu ya White House -- iliyozungushiwa na utepe wa polisi-- na kwenye jengo la taifa karibu na hapo walionekana kuweza kukubaliana juu yake lilikuwa kwamba hivyo sivyo walivyotaka mambo yawe.

"Tunapaswa kusherehekea umoja wetu, utofauti wetu, uhuru, hatupaswi kuangaliana kama maadui walio tayari kwenda vitani," mwanaharakati anaemuunga mkono Trump Kristy Pandora Greczowski aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP.

Mary Byrne, 54, alikuja na watoto wawili wa kiume, alisema ana wasiwasi kuhusu uhasama uliopo sasa. "Hatuzungumzishani tena, tunakaripiana. Tunahitaji kutazama ndani kuona tatizo letu," alisema.

Kwa muda mrefu Wamarekani wamegawika kwa misingi ya maadili ya kiliberali na kihafidhina. Lakini madhara makubwa ya janga la virusi vya corona yamesababisha hofu kubwa na wasiwasi.

USA, Washington I Donald Trump I Salute to America
Sherehe za Saluti kwa Marekani za mwaka 2020 zilifanyika katika uwanja wa kusini wa ikulu ya White House kuadhimisha siku ya Uhuru wa Marekani, Julai 4, 2020.Picha: Imago Images/K. Cedeno

Kisha, mnamo mwezi Mei, mwanaume wa Kimarekani mwenye asili ya Afrika aliuliwa na afisa wa polisi mzungu mjini Minneapolis, na kuzusha wimbi la maandamano.

Tangu wakati huo, Marekani imeanza kujitathmini kuhusu historia yake ya ubaguzi, dhulma za sasa za ubaguzi --- zikiwemo zile zinazozidi kumulikwa na athari za virusi vya corona na ukatili wa polisi.

Rais asiejali kuwagawa zaidi raia

Trump, akiwa mbali na kuhimiza maridhiano ya kitaifa, amezidi kuchochea tu migawiko.

"Kamwe hatutoruhusu kundi la watu wenye hasira kuvunja masanu yetu, kufuta historia yetu, kuwaja itikadi watoto wetu au kukanyaga uhuru wetu," alikiambia kikundi cha watu kwenye uwanja wa ikulu Jumamosi jioni.

Mapema, kwenye mtaa ulioko nje ya White House, Jennifer Friend alisema rais "anakosewa heshima."

"Maisha yote yana thamani, lakini waandamanaji wanachagua kila wanachotaka kuandamana juu yake. Ni unafiki," alisema mtalii huyo mwenye umri wa miaka 53 kutoka Florida.

Zaidi kwenye jengo la taifa lililokuwa na joto kali la jua, Katima McMillan, 24, kutoka Kentucky, alikuwa na kundi la wanaharakati.

Kwenye uwanja, walisambaza mipira nyumbufu ya rangi tatu za uafrika: nyekundu ikiwakilisha damu iliomwagika katika mapambano ya ukombozi, nyeusi inayowakilisha watu wa bara, na kijani inayowakilisha utajiri wa asili wa Afrika.

USA, Washington I Donald Trump I Salute to America
Rais Trump akiinua ngumi yake baada ya kuwasili kwa ajili ya tukio la "Saluti kwa Marekani" la 2020 kuadhimisha siku ya uhuru wa taifa hilo mjini Washington, DC, Julai 4, 2020.Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb

"Hatutofautiani na mtu yeyote mwingine, haki za watu weusi ni haki za binadamu," alisema kijana huyo Mmarekani mwenye asili ya Afrika.

Lakini kulikuwepo na wale ambao dhamiri yao ya kuifurahia siku hiyo ya mapumziko bila kujali lolote ilitoa mwanga wa matumaini kwamba taasisi za Marekani huenda zikahimili migawiko.

Wayne na Lynnis, wapenzi kutoka Maryland, walikuwa miongoni mwa wageni waliochaguliwa kuhudhuria hotuba ya Trump iliyopewa jina la "Saluti kwa Marekani" kwenye uwanja wa ikulu ya White House.

"Nimesisimuka" alisema Lynnis mwenye umri wa miaka 56.

"Sijali nani yuko madarakani, ni heshima kutembelea ikulu ya nchi yako," aliongeza kwa tabasamu.

Chanzo: AFPE