1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Marekani yaonyesha wasiwasi kuhusu hali ya kiutu Gaza

Grace Kabogo
5 Machi 2024

Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya kiutu katika Ukanda wa Gaza,

https://p.dw.com/p/4dB1w
Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris
Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala HarrisPicha: Johannes Simon/Getty Images

Akizungumza Jumatatu na Benny Gantz mjumbe wa ngazi ya juu wa baraza linalosimamia vita nchini Israel mjini Washington, Kamala Harris amesema hali ya kibinadamu huko Gaza inatisha ambapo zaidi ya Wapalestina 100 waliuawa wakati wakijaribu kupokea misaada iliyopelekwa katika ukanda huo.

Harris ameitolea wito Israel kuchukua hatua zaidi kuongeza na kurahisisha upatikanaji wa misaada.

Marekani yaitaka Hamas kukubali masharti yaliyopo

Taarifa ya Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa Harris pia amewatolea wito wapiganaji wa Hamas kukubali masharti yaliyoko mezani ambapo kuachiliwa kwa mateka, kutasababisha kusitishwa vita mara moja kwa muda wa wiki sita na kuwezesha misaada ya kiutu kuingia Gaza.

Marekani, Israel na nchi nyingine kadhaa zimeliorodhesha kundi la Hamas kuwa la kigaidi. Ziara ya Gantz nchini Marekani inafanyika huku kukiwa na msuguano kati ya Marekani na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuhusu jinsi ya kupunguza mateso ya Wapalestina huko Gaza na mpango wa baada ya vita kwenye eneo hilo.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayehusika na unyanyasaji wa kingono katika mizozo, Pramila Patten
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayehusika na unyanyasaji wa kingono katika mizozo, Pramila PattenPicha: Lev Radin/Sipa USA/picture alliance

Wakati huo huo, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia unyanyasaji wa kingono katika maeneo yenye mizozo, Pramila Patten amesema kuna mazingira ya kuaminika yanayoonesha kuwa wapiganaji wa Hamas walifanya ubakaji, unyanyasaji wa kingono na unyanyasaji mwingine wa kinyama dhidi ya wanawake katika shambulizi la Oktoba 7 kusini mwa Israel.

Unyanyasaji wa kingono bado unaendelea

"Kuhusu mateka waliopelekwa Gaza. Tulipata taarifa za wazi na zenye kushawishi kwamba unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo utesaji, ukatili, unyanyasaji wa kingono na udhalilishwaji umefanywa dhidi ya mateka. Na pia tuna sababu za kuridhisha kuamini kwamba huenda ukatili kama huo bado unaendelea dhidi ya wale ambao bado wamezuiliwa," alifafanua Pramila.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kufanyika uchunguzi zaidi, akisisitiza kwamba ugunduzi huo hauhalalishi ghasia zaidi kwa njia yoyote ile, lakini kwa hakika unatilia mkazo haja ya mapigano kusitishwa haraka.

Helikopta ya Israel ikiwa kuisni mwa Israel
Helikopta ya Israel ikiwa kuisni mwa IsraelPicha: Ohad Zwigenberg/AP Photo/picture alliance

Ama kwa upande mwingine, jeshi la Israel imelishutumu shirika la Umoja wa Mataufa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA kwa kuwaajiri mamia ya wanamgambo katika Ukanda wa Gaza. Jeshi hilo limesema Israel tayari imeujulisha Umoja wa Mataifa kuhusu taarifa hizo.

Msemaji wa jeshi la Israel, Daniel Hagari amesema zaidi ya wafanyakazi 450 wa UNRWA ni watendaji wa kijeshi ndani ya vikundi vya kigaidi huko Gaza. Amesema idadi hiyo sio ya bahati mbaya, bali ni utaratibu uliopo.

Juhudi za kidiplomasia za kusitisha mapigano Gaza zaongezeka

Huku hayo yakijiri, wapatanishi wa kimataifa na wajumbe wa Hamas wanaendelea na mazungumzo mjini Cairo, Misri, kwa lengo la kujaribu kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda katika Ukanda wa Gaza, kabla ya kuanza kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhani mapema wiki ijayo.

Wajumbe wa Hamas na wale wa Marekani, wanatarajia kukutana na wapatanishi kutoka Qatar na Misri katika siku ya tatu ya majadiliano ya kufikia makubaliano ya kusitisha vita kwa wiki sita.

 

(AP, AFP, Reuters)