1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaonywa juu ya kuhamishia ubalozi wake Jerusalem

Isaac Gamba
4 Desemba 2017

 Jumuiya ya nchi za kiarabu, Palestina  na Jordan zimeionya Marekani dhidi ya uamuzi wake wa kuhamishia ubalozi wake mjini Jerusalem. 

https://p.dw.com/p/2oiCn
Israel | Palästina Jerusalem - Felsendom
Picha: picture alliance/dpa/R.Holschneider

Jumuiya hiyo ya nchi za kiarabu imesema hatua hiyo inaweza ikakwamisha mazungumzo yoyote ya siku zijazo na pia inaweza ikasababisha kuibuka tena vurugu katika kanda ya Mashariki ya Kati. 

Onyo hilo linakuja mnamo wakati rais wa Marekani Donald Trump akifikiria kufanya uamuzi wa kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka mjini Tel Aviv hadi Jerusalem, hatua ambayo itakuwa inaashiria kuutambua rasmi mji huo wa kale kama mji mkuu wa Israel. Mji huo unagombaniwa kati ya Israel na Palestina.  Uamzi huo wa Marekani kuhusiana na hatua hiyo unaweza ukatolewa leo Jumatatu.

Naabil Shaath ambaye ni mshauri mwandamizi wa rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina  Mahmoud Abbas alinukuliwa akisema hapo jana kuwa " Tumeionya Marekani kuwa kama serikali ya nchi hiyo itathubutu kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel  na kuhamishia ubalozi wa Marekani katika mji huo basi hii itakua ni hatua itakayofikisha mwisho fursa ya mazungumzo ya amani"

Kwa upande mwingine, katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu  Ahmed Aboul Gheit amesisitiza juu ya onyo hilo na kusema hatua hiyo ya Marekani haitasaidia kuleta amani au uthabiti bali itachochea vurugu na pia kunufaisha upande mmoja ambao ni serikali ya Israel.

Waziri wa mambo ya nje wa Jordan Ayman Safadi ambaye amesema ameibua swala hilo katika mazungumzo yake na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson.

Safadi  aliandika katika ukurasa wa twitter kuwa uamuzi kama huo utaibua hasira miongoni mwa jamii ya waislamu katika mataifa ya kiarabu, kuchochea mivutano na kuvuruga juhudi za amani. 

 

Trump bado kutoa uamuzi

USA Präsident Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/J. L. Duggan

Hapo jana Jumapili  mshauri wa rais Donald Trump kuhusu Mashariki ya Kati  Jared Kushner ambaye amepewa jukumu  la kuongoza juhudi za Marekani katika mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina amesema rais Trump bado  hajafanya uamuzi kuhusiana na hatua hiyo.

Rais Trump anaripotiwa kufikiria kutoa uamuzi kuhusiana na suala hilo  mapema iwezekanavyo kabla ya Jumatano wiki hii.

Marekani kwa muda mrefu imekua ikisema kuwa suala linalohusiana na hadhi ya mji wa Jerusalem ambao pande zote za Israel na Palestina  zinadai kuwa ni mji mkuu wake ni lazima liamuliwe kama sehemu ya mchakato wa amani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la mamlaka ya ndani ya Palestina Wafa , rais Mahmoud Abbas  amewaonya viongozi wa Jumuiya ya kimataifa kuwa uamuzi huo utapelekea ukanda huo kuingia katika machafuko ambayo suluhu yake itakua vigumu kupatikana.

Israel imekua ikiichukulia Jerusalem kua ni mji wake mkuu na kwa muda mrefu imekua ikiitaka Marekani kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv na kuupeleka katika mji huo huku serikali ya Mamlaka ya Palestina nayo pia ikisema Jerusalem Mashariki utakua mji mkuu wa taifa la baadaye la Palestina.

Mwandishi: Isaac Gamba/dw/dpae/afpe

Mhariri :Caro Robi