1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaruhusu tena wakimbizi kutoka nchi 11

Zainab Aziz
30 Januari 2018

Marekani itaanza tena kuwaruhusu wakimbizi kutoka nchi 11 zinazozingatiwa kuwa za hatari kubwa kwa usalama. Lakini mchujo mkali utafanyika kwa watu hao kutoka hasa Mashariki ya Kati na Afrika kabla ya kuingia Marekani.

https://p.dw.com/p/2rkSR
USA Syrische Flüchtlinge sind für ein Tag Touristen in New Yorker
Picha: Getty Images/AFP/D. Emmert

Mabadiliko hayo yamefanyika baada ya miezi mitatu ya uchunguzi uliofanywa na wizara ya mambo ya nje, wizara ya mambo ya ndani na mashirika ya ujasusi juu ya wakimbizi kutoka Misri, Iran, Libya, Mali, Korea Kaskazini, Somalia, Sudan na Yemen.

Sheria hizo mpya ni mabadiliko ya hivi karibuni yaliyofanywa na utawala wa Rais Donald Trump katika mpango wa wakimbizi nchini Marekani kwa lengo la kuzingatia maslahi ya usalama ya nchi hiyo. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na utawala wa Trump, ikiwa pamoja na kuwapiga marufuku kwa muda, wakimbizi wote kuingia Marekani zilisababisha vita virefu vya kimahakama.Watetezi wa wakimbizi wamesema wanaziona hatua za serikali ya Marekani kuwa na lengo la kupunguza idadi ya wakimbizi kutoka hasa nchi za Kiislamu.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture-alliance/dpa/NOTIMEX/Casa Blanca

Rais Trump leo anatarajiwa kutoa hotuba yake ya kwanza juu ya hali ya taifa na amesema suala la uhamiaji atalizungumzia pia katika hotuba yake ya leo. Afisa mwandamizi ambaye hakutaka jina lake litajwe aliwafahamisha waandishi habari juu ya mabadiliko hayo mapya na amesema hatua hizo ni za kiusalama. kwa mujibu wa uchunguzi wa shirika la habari la Reuters kuhusu takwimu za wizara ya mambo ya ndani wakati wa kipindi cha mapitio tokea mwishoni mwa mwezi Oktoba hadi wiki iliyopita, idadi ya wakimbizi kutoka nchi hizo 11 zinazozingatiwa kuwa ni za hatari waliotaka kuingia Marekani imepungua kwa kiwango kikubwa.

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama
Rais wa zamani wa Marekani Barack ObamaPicha: Reuters/M. Makela

Marekebisho juu ya orodha ya "nchi za hatari" kwa mara mwisho yalifanywa wakati wa utawala wa Rais Barack Obama mnamo mwaka 2015. Tangu alipochukua hatamu za uongozi Rais Trumb ametoa matamko ya aina mbalimbali ya kupiga marufuku kwenye mipango ya wakimbizi ikiwa ni pamoja na kuweka idadi mahususi ya wakimbizi watakaoruhusiwa kuingia nchini Marekani ambayo ni zaidi ya nusu ya ile iliyowekwa na mtangulizi wake Barack Obama kwa mwaka 2017.

Pia Trump alitoa amri ya kiutendaji ya kusimamisha mpango wa wakimbizi hadi ufanyiwe mapitio ya kina pamoja na kuweka amri hiyo ya mchujo mkali kwa wakimbizi kwa ajili ya kukabiliana na suala la uhamiaji duniani.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani tangu tarehe 25 mwezi Oktoba siku ambayo ulianza muda wa siku 90 wa zuio la wakimbizi kutoka nchi hizo 11, wakimbizi 46 wameruhusiwa kuingia nchini Marekani.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/DPA

Mhariri: Grace Patricia Kabogo