1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasema Urusi ilituma ndege za kijeshi Libya

26 Mei 2020

Kamandi ya jeshi la Marekani barani Afrika, AFRICOM, imesema Urusi ilituma ndege zake za kijeshi nchini Libya ili kuwaunga mkono mamluki kutoka Urusi wanaomsaidia kamanda wa vikosi vya jeshi la mashariki Khalifa Haftar.

https://p.dw.com/p/3cnAg
SU-35 fighter Jet
Picha: picture-alliance/dpa/TASS/M. Lystseva

Ndege hizo zilitoka Urusi na kutua kwanza Syria ambako zilibadilishwa rangi ili kuficha alama za nchi zilizotokea kabla ya kuwasili Libya, inaelezea taarifa ya AFRICOM yenye makao yake makuu yake Stuttgart, Ujerumani.

Jeshi la Marekani halikuweka wazi lini ndege hizo ziliwasili, likielezea tuu kwamba ni hivi karibuni.

Libyen Haftar Truppen Angriff Mitiga Airport in Tripolis
Picha: picture-alliance/AA/H. Turkia

Taarifa hiyo imejiri siku moja baada ya serikali ya mpito ya mjini Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kusema kwamba mamia ya mamluki kutoka Urusi wanaomuunga mkono jenerali Haftar waliondolewa kwenye maeneo ya vita ya kusini mwa Tripoli.

Kujiondoa huko kunatokana na juhudi za bila mafanikio za Jenerali Haftar za kutaka kuuteka mji wa Tripoli kwa miaka kadhaa sasa. Serikali ya Urusi imekuwa ikikanusha kuhusika katika vita hivyo.

Lakini ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa mwezi uliopita inaelezea kwamba kampuni ya Wagner, yenye uhusiano wa karibu na rais wa Urusi Vladimir Putin, iliwatuma mamluki ili kumsaidia Haftar.

Urusi imekanusha madai hayo kwa muda mrefu 

Libyen Tripoli | Portrait | GNA Kämpfer
Picha: picture-alliance/dpa/A. Salahuddien

Kwa muda mrefu Urusi imekanusha kuhusika katika mzozo unaondelea Libya, lakini kwa sasa haiwezi tena kukanusha, alisema Jenerali Stephen Wownsend wa jeshi la Marekani kwenye kikosi cha AFRICOM.

Aliendelea kusema kwamba kama inavyofanya huko Syria, Urusi inawapeleka pia mamluki wake wanaoungwa mkono na serikali barani Afrika kwa kutumia makundi kama Wagner.

Uvamizi wa jeshi la kimataifa umeongeza mzozo huo huku Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Urusi zikimuunga mkono Haftar na Uturuki ikiiunga mkono serikali ya Tripoli.

Libya imekuwa katika hali ya vurugu tangu kuangushwa kwa utawala wa kiongozi wa muda mrefu, Moamer Gaddafi wakati wa mapinduzi yaliyoungwa mkono na Jumuia ya kujihamu ya NATO mwaka 2011.

Mwandishi : Saleh Mwanamilongo/ AFPE

Mhariri : Grace Patricia Kabogo