1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasimamisha mashirikiano na Urusi kuhusu Syria

Mohammed Khelef
4 Oktoba 2016

Wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likisaka makubaliano mapya ya kuendeleza usitishaji mapigano nchini Syria, Marekani imesitisha mashirikiano yake na Urusi ikiilaumu kuendelea kuwashambulia raia.

https://p.dw.com/p/2QqcY
USA Russland Diplomatie John Kerry US Außenminister
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. DeCrow

Msemaji wa ikulu ya Marekani, Josh Earnest, msemaji wa wizara ya mambo ya nje, John Kirby, na mwenzake Elizabeth Trudeau, kwa nyakati tafauti wameelezea msimamo unaowiana juu ya kile wanachosema ni kusitishwa kwa mashirikiano ya pande mbili kuelekea mzozo wa miaka mitano nchini Syria, kati ya nchi yao na Urusi. 

Wakati Earnest wa Ikulu ya White House akisema "kila mmoja ameshachoshwa na kuivumilia Urusi", Kirby wa Mambo ya Nje amesema "huu umekuwa uamuzi mgumu kabisa kuchukuliwa, lakini ambao umebidi."

Akisoma tamko rasmi la serikali ya Marekani mbele ya waandishi wa habari, Elizabeth Trudeau, amesema hakuna njia ambapo Marekani sasa inaweza kushirikiana tena na Urusi, kwani malengo yao yanapingana.

"Kwa bahati mbaya, Urusi imeshindwa kuheshimu ahadi zake, ikiwemo wajibu wake chini ya sheria za kimataifa na Azimio Namba 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaloidhinisha mpango wa amani wa Syria.

Pia haikuwa tayari ama haikuweza kuhakikisha kuwa utawala wa Syria unatekeleza mipango ambayo awali Moscow iliikubali, na badala yake Urusi na Syria zimechagua kutumia njia za kijeshi kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano," alisema Trudeau.

Hadi sasa hakuna lolote lililosemwa kuwa ni mpango mbadala kutoka upande wa Marekani, licha ya kuwepo uvumi kwamba huenda sasa itachukuwa hatua kali zaidi dhidi ya Urusi, na pia washirika wake katika mataifa ya Ghuba, yaani Saudi Arabia na Qatar, huenda wakatuma shehena za silaha kwa waasi wanaoupinga utawala wa Bashar al-Assad nchini Syria.

Urusi yasema iko sahihi 

Lakini kwa upande wa Urusi, msimamo wake uko wazi, nao ni kuendelea kuusaidia utawala wa Assad kuikomboa nchi nzima kutoka mikononi mwa wale inaowaita "makundi ya kigaidi".

USA UN Sicherheitsrat Sitzung zu Ukraine in New York Witali Tschurkin
Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin.Picha: Reuters

Balozi wa nchi hiy kwenye Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, ambaye ndiye rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu, amewaambia waandishi wa habari kwamba hata kama Marekani inakatisha mashirikiano yake, msimamo wa Urusi ni sahihi.

"Lau si kujiingiza kwetu Syria, leo bendera nyeusi za IS zingelikuwa zinapepea kote Damascus. Huo ndio ukweli wa hali ilivyo. Na huu ndio ukweli wa mambo kwamba kundi la Nusra limeelekea mashariki mwa Aleppo. Umoja wa Mataifa, Stefan de Mistura, amesema wazi kwenye Baraza la Usalama kwamba nusu ya wapiganaji walioko huko ni Nusra. Wamewakamata raia mateka huko," alisema Churkin.

Tayari Urusi imeipinga rasimu ya azimio la kukomesha mapigano ya Aleppo iliyowasilishwa na Ufaransa kwenye Baraza la Usalama, ikisema hakuna kinachoweza kufikiwa kabla ya kwanza kuwamaliza magaidi walioko huko. 

Na wakati Marekani zikivutana, mpatanishi wa Umoja wa Mataifa kwenye mzozo wa Syria, Steffan de Mistura, amerejelea msimamo wake kuwa hajavunjika moyo na kupatikana kwa amani, ingawa hadi sasa uhalisia uko dhidi yake. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga