1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Marekani yatishia mashambulizi zaidi Mashariki ya Kati

John Juma
5 Februari 2024

Marekani imetishia kufanya mashambulizi zaidi ya kulipiza kisasi endapo wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran katika Mashariki ya Kati wataendelea na mashambulizi yao.

https://p.dw.com/p/4c2yu
Mashambulizi ya Marekani dhidi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran ni ya kulöipiza kisasi dhidi ya vifo vya wanajeshi wake watatu waliouawa kwenye shambulizi Iraq.
Mashambulizi ya Marekani dhidi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran ni ya kulöipiza kisasi dhidi ya vifo vya wanajeshi wake watatu waliouawa kwenye shambulizi Iraq.Picha: U.S. Central Command/Handout via REUTERS

Onyo la Marekani kwa Iran na wanamgambo inaowahami wakiwemo waasi wa Kihouthi wa Yemen, limejiri mnamo wakati Marekani imefanya mashambulizi dhidi ya vituo kadhaa vya wanamgambo ndani ya Syria na Iraq mwishoni mwa juma.

Ripoti za wanamgambo hao zimeeleza kuwa zaidi ya vituo 85 vilishambuliwa katika maeneo saba. Miongoni mwa vituo vilivyoshambuliwa ni pamoja na kamandi, na makao makuu ya operesheni, vituo vya intelijensia, maghala ya roketi, makombora, droni, risasi na vituo vingine vinavyohusishwa na wanamgambo au Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Qud, kitengo kinachoshughulikia uhusiano wa Iran na kuwapa wanamgabo silaha.

Soma pia: Waasi wa Kihuthi waapa kujibu mashambulizi ya anga ya Marekani na Uingereza

Ulipizaji kisasi wa Marekani ulichochewa na mashambulizi ya wanamgambo yaliyowaua wanajeshi watatu wa Marekani katika kambi yao nchini Jordan siku kadhaa zilizopita. Hapo jana Jumapili, Marekani iliwafyatulia risasi tena Wahouthi.

Jake Sullivan, mshauri wa rais wa Marekani Joe Biden kuhusu masuala ya usalama wa taifa amesema Iran inapaswa kutarajia jibu kali na la haraka ikiwa yenyewe au washirika wake wataamua kufanya mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya Marekani na vituo vyake.

Soma pia: Wahouthi wafyatua makombora kuelekea meli za kivita za Marekani

"Siwezi kukuambia kwamba Tehran imebadilisha sera yake. Ninachoweza kukuambia ni jinsi mbinu ya Marekani itakavyokuwa, ambayo ni kwamba ikiwa tutaendelea kuona vitisho na mashambulizi kutoka kwa makundi haya ya wanamgambo, tutawajibu na tutawawajibisha wale waliohusika," amesema Sullivan.

Marekani imetishia kuzidisha mashambulizi ikiwa Iran au wanamgambo inaowaunga mkono watathubutu kushambulia Marekani au vituo vyake.
Marekani imetishia kuzidisha mashambulizi ikiwa Iran au wanamgambo inaowaunga mkono watathubutu kushambulia Marekani au vituo vyake.Picha: AS1 Jake Green/AP Photo/picture alliance

Israel yawaua wanamgambo kadhaa wa Hamas

Katika tukio jingine,  vikosi vya kijeshi vya Israel vimewaua wanamgambo zaidi wa kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Soma pia: Mzozo wa Gaza watishia kutanuka kote Mashariki ya Kati

Jeshi hilo lilisema ndege ya kivita pia ilimuua mshambuliaji mlenga shabaha wa kundi hilo lenye itikadi kali za dini ya Kiislamu.

Jeshi la Israel limeeleza zaidi kwamba wanajeshi wake walifanya operesheni katika kituo kinachotumiwa na kamanda wa Hamas kilichoko eneo hilo la Khan Younis, na kupata bunduki, risasi na zana nyingine za kijeshi vikiwemo pia vifaa vya kiufundi.

Jeshi lake la majini pia lilishambulia maeneo ya Hamas na kuvisaidia vikosi vya ardhini.

Israel ilianzisha vita dhidi ya wanamgambo wa Hamas, baada ya kundi hilo kufanya shambulizi baya Oktoba 7, kusini mwa Israel, na kuua watu 1,200 na kushika wengine takriban 250 mateka.

Soma: Umoja wa Ulaya watahadharisha usitishaji msaada UNRWA

Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine kadhaa zimeliorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.

Kulingana na wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, zaidi ya Wapalestina 27, 360 wameuawa na vikosi vya Israel katika Ukanda wa Gaza tangu vita hivyo vilipoanza.

Kwa sasa Israel imeimarisha operesheni yake ya kijeshi huko Khan Younis, eneo linalotizamwa kuwa ngome ya wanamgambo. Hayo yamesemwa na jeshi hilo.
Kwa sasa Israel imeimarisha operesheni yake ya kijeshi huko Khan Younis, eneo linalotizamwa kuwa ngome ya wanamgambo. Hayo yamesemwa na jeshi hilo.Picha: Ramez Habboub/AP Photo/picture alliance

Israel yashambulia vituo vya Hezbollah kusini mwa Lebanon

Baadaye Jumapili, jeshi la Israel lilisema lilifanya mashambulizi mapya dhidi ya wanamgambo wa Kishia Hezbollah, kusini mwa Lebanon.

Kulingana na kauli ya jeshi hilo, ndege zake zilipiga kituo kinachotumika kama kamandi ya Hezbollah na pia kituo cha kijeshi katika Kijiji cha Yaroun.

Hata hivyo taarifa hiyo haikuweza kuhakikiwa nya vyombo huru.

Tangu vita vya Gaza vilipoanza, kumekuwa na makabiliano ya mara kwa mara kati ya jeshi la Israel na makundi ya wanamgambo kama Hezbollah karibu na mpaka wa Israel na Lebanon.

Marekani imeonya kuwa itazidisha mashambulizi ya kulipiza kisasi, endapo wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran wataendelea na mashambulizi yao.

Vyanzo: APE, DPAE, EBU