1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yatumia kura ya turufu kupinga azimio la Gaza

Bruce Amani
21 Februari 2024

Marekani imetumia kura ya turufu kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotoa wito wa kusitishwa mapigano katika eneo hilo la Kipalestina. Hayo ni wakati mashambulizi ya Israel yakiendelea huko Gaza

https://p.dw.com/p/4cdYL
Mkutano wa kupigia kura azimio la kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza
Marekani inasema rasimu hiyo itaathiri mazungumzo ya kuwachiwa mateka na kusitishwa mapigano kwa mudaPicha: Seth Wenig/AP Photo/picture alliance

Washington ilipinga rasimu ya kwanza iliyotayarishwa na Algeria, ambayo ilitaka kusitishwa mara moja kwa mapigano kwa ajili ya kupelekwa misaada ya kiutu na kuwachiwa bila masharti kwa mateka wote waliokamatwa katika shambulizi la Oktoba 7.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Lind Thomas-Greenfield alisema rasimu hiyo itaathiri vibaya mazungumzo nyeti kuhusu mpango wa mateka na kusitishwa kwa mapigano angalau kwa wiki sita.

Kundi la Hamas linasema kura ya turufu ya Marekani ni sawa na kutoa idhini kwa Israel kuendelea na maangamizi zaidi. Kura hiyo ilichochea ukosoaji kutoka kwa nchi zikiwemo China, Urusi, Saudi Arabia na hata washirika wa karibu wa Marekani wakiwemo Ufaransa na Slovenia.

Wakati mvutano wa kidiplomasia ukiendelea, Israel iliipiga Gaza na makombora ya angani na ardhiniambayo yamewauwa Wapalestina zaidi ya 103 katika kipindi cha saa 24. Wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas imesema mashambulizi ya Israel yaliendelea Jumanne usiku ambapo pia mji wa kusini wa Rafah ulilengwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani - WFPlimesitisha shughuli za usambazaji wa bidhaa muhimu za chakula kaskazini mwa ukanda wa Gaza hadi pale hali ya usalama itakaporuhusu tena kuendelea kwa zoezi hilo.