1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marufuku kuzomea wimbo wa Taifa

16 Oktoba 2008

Ufaransa ni marufuku kuzomea wimbo wa Taifa unapopigwa uwanjani.

https://p.dw.com/p/FbPe

Mipango ya FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni kuweka viwango maalumu vya wachezaji wa kigeni wanaochezea klabu za nje ,ni hatua nzuri kwa mchezo wa dimba ,lakini hautafanikiwa-Dino Zoff, kipa mashuhuri wa zamani wa timu ya Taifa ya Itali amesema.

Mjadala motomoto umezuka nchini Ufaransa baada ya rais Nicolas Sarkozy kuamua kuvunjwa mashindano yoyote ya dimba ambamo mashabiki wanazomea wimbo wa Taifa unapopigwa.Kisa kama hicho kilitokea kati ya wiki hii pale Ufaransa ilipocheza na Tunisia.

Rais wa FIFA Sepp Blatter ameungwamkono mpango wake wa kanuni ya wachezaji 6 wa nyumbani na 5 wa kigeni ambao utapunguza idadi ya wachezaji wa nje wanaoteremshwa uwanjani mechi inapoanza.Aliitoa kanuni hiyo wakati wa mkutano mkuu wa FIFA hapo Mei. Hatahivyo, mpango huo unagongana na kanuni za Umoja wa Ulaya zinazotoa uhuru wa wafanyikazi wa nchi zanachama kutumika watakako.Kipa wa zamani wa taifa wa Itali Dino Zoff, haoni jinsi gani FIFA itaweza kukiuka kanuni hiyo.

Ulimwengu ni wa utandawazi na hivyo ni vigumu kabisa kuweka mipaka kwa wachezaji wa kigeni-alisema mzee Dino zoff mwenye umri wa miaka 66 hivi sasa.

Zoff alisema amefurahishwa kuona mtindo wa Premier League-Ligi ya Uingereza - wa timu za huko zanunuliwa na matajiri wa kigeni, haukufikia bado Serie A -Ligi ya Itali.

Alitumai zoff,nahodha wa timu ya Itali iliotwaa kombe la dunia, 1982, kuwa hali itabakia hivyo nchini Itali.Zoff akizungumza katika makao makuu ya Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) mjini Roma kabla hafla ya kupambana na njaa ulimwenguni.

Wakati hali ni hivyo nchini Itali kwa mabingwa wa dunia, nchini Ufaransa kwa makamo-bingwa mjadala motomoto umezuka huko baada ya Rais wa Ufaransa Nicholas sarkozy kuamua atavunja mechi yoyote ambamo mashabiki watazomea pale wimbo wa taifa unapopigwa.

Uamuzi huo ulitangazwa juzi na waziri wa michezo wa Ufaransa Roselyne Bachelot baada ya mashabiki wa Tunisia walipozomea uwanjani pale wimbo wa taifa wa Ufaransa ulipoimbwa na muimbaji wa ktunisia kabla Ufaransa kupambana na Tunisia kwa dimba la kirafiki katika uwanja wa Stade de France,mjini Paris.

Rais Sarkozy aliueleza mkasa huo kuwa ni "aibu" na akamuita Ikulu Elysee Palace rais wa shirikisho la dimba la Ufaransa kwa kikao maalumu.Uamuzi ukapitishwa kuvunja mechi zozote mkasa kama huo ukitokea.

Kisa hicho cha kuzomewa wimbo wa taifa si cha kwanza nchini Ufaransa.Hapo Mei 2002, rais wa zamani wa Ufaransa Jacques Chirac aliondoka uwanja huo huo wa Stade de France kabla ya finali ya kombe la Taifa la Ufaransa pale wimbo wa Taifa ulipozomewa na mashabiki wa klabu ya Bastia ya kisiwa kinacholilia uhuru cha Corsica.

Baadhi ya mashabiki wa Tunisia walioshiriki katika kisa cha juzi wamedai kuzomea kwao hakujamlenga yeyote."Ni desturi ya mashabiki wa nchi za Maghreb kufanya hivyo"-kijana mmoja aliiambia radio Info-radio.

Wachezaji wa timu ya Ufaransa,hawakuonesha kuudhika sana na kisa hicho.Mchezaji wa kiungo Hatem Ben Arfa wa asili ya tunisia , alisema kisa hicho sio kibaya hivyo.Chipukizi wale ni watunisia na wakitaka kujionesha ni watunisia.Inabidi kuwaelewa tu.

Vyombo vya habari vya ufaransa, havioneshi kuridhika na uamuzi huo wa kuvunja mechi endapo wimbo wa Taifa ukizomewa.Lakini pia havipendezwi na mtindo wa kuzomea wimbo wa taifa unapopigwa. Na gazeti la Paris Normandie lauliza: Firimbi ngapi au mara ngapi mtu akizomea itastahiki kuvunja mechi na kuwaondoa uwanjani mashabiki ?