1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Masaa mengine 72 ya kuweka silaha chini Gaza yaanza

Admin.WagnerD11 Agosti 2014

Masaa mengine 72 ya kusitisha mapigano yameanza kutekelezwa tena mjini Gaza, wakati wajumbe wa timu ya upatanishi kati ya Isreal na Palestina wakiwasili mjini Cairo, Misri kwa ajili ya kutafuta suluhu ya muda mrefu.

https://p.dw.com/p/1CsPK
Wanajeshi wakipunzika baada ya kutangazwa mapumziko ya masaa 72
Picha: REUTERS

Hatua hiyo ya kusimamisha mapigano,iliyoanza usiku wa kuamkia leo inatokana na matunda ya mkutano wa siku kadhaa wa upatanishi uliyochini ya usimamizi wa Misri, ambao umekuwa na lengo la kufikisha kikomo machafuko hayo ambayo mpaka sasa yamesasabisha vifo vya Wapalestina 1,939 na Waisrael 67 tangu Julai 8.

Ikiwa imezidi masaa 10 tangu kuanza kutelezwa kwa hatua hiyo anga ya Ukanda wa Gaza imekuwa kimya kabisa pasipokuwepo kwa ripoti yoyote ya vurugu kutoka katika pande tofauti za eneo hilo. Dalili za nuru mpya ya kurejea kwa hali ya kimaisha imeanza kuonekana katika maeneo hayo ambayo ni makazi ya watu milioni 1.8.

Asubuhi ya kwanza ya masaa 72 Gaza

Asubuhi ya leo jua lilichomoza Gaza City, wenye maduka na biashara mbalimbali walionekana kufungua milango yao. Na idadi fulani ya watu vilevile ilionekana kuingia madukani kwa ajili ya kujipatia bidhaa mbalimbali. Nje ya jengo la shule moja inayoendesha na Umoja wa Mataifa idadi kadhaa ya magari na mikokoteni inayokokotwa na punda imeonekana ikisubiri wakimbizi waliokuwa wakijihifadhi hapo ili waweze kuwarejesha majumbani mwao.

Gaza Waffenruhe 11.08.2014
Asubuhi ya masaa ya mwanzo ya kusitisha mapigano GazaPicha: Reuters

Shirika la habari la Ufaransa AFP limenukuu mkimbizi mmoja Hikmat Atta akisema" Tunataka kurejea majumbani mwetu kwenda kuona kipi kilichotokea huko" Bwana huyo akiwa katika gari dogo na familia yake alikuwa akielekea nyumbani kwake mji wa kaskazini wa Beit Lahiya ambako alikimbia siku ya kwanza kabisa baada ya kuanza kwa vita hivyo.

Lakini vilevile aliongeza kwa kusema kwamba wanarejea nyumbani kwa siku hii ya kwanza na baadae wanaweza kurudi kambini kwa vile utekelezaji ndio wa kusitisha mapigano upo katika hatua ya awali kabisa kwa hivyio bado wana wasiwasi.

Isreal yatoa onyo

Mark Regev ni msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu ya Isreal. "Tumekubali na kuheshimu hatua muhimu nane za kusitisha mapigano, hatua ambazo Hamas waliweza kukaidi au kuzivuruga. Na kama Hamas watavurugu vilevile hatua hii ya sasa, hatusita kuchukua hatua kuwalinda watu wetu kutokana na mashambulizi ya kigaidi ya Hamas"

Misri imezitaka pande zinazohasimiana- Isreal na Hamas katika siku hizi tatu kufikia makubaliano ya kina na ya kudumu baada ya jitihada kama hizo kushindwa ijumaa iliyopita kufuatia na kuanza upya mapambano. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema hii itaoa fursa nyingine ya kusitisha mapigano ya muda mrefu huku akisisitiza jitahda za kushughulikia malalamiko ya msingi baina ya pande zote mbili.

Kiongozi wa Hamas anaeishu uhamishoni, Khaled Meshaal aliliambia shirika la habari la AFP katika mahojiano maalum hapo jana, kwamba lazima Israel iache kuuzingira ukanda wa Gaza kulikodumu kwa miaka minane sasa.

Mpatanishi mkongwe wa Palestina Saeb Erakat amewasili mjini Cairo jana jioni kwa ajili ya mazungumzo na Misri na wajumbe wa Jumuiya ya Kiarabu. Huyo anamwakilisha rais Mahmud Abbas. Wakati huo huo timu upatanisha kutoka upande wa Israel nayo imewasili mjini humo leo hii.

Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri: Josephat Charo