1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio Afghanistan

Oumilkher Hamidou10 Agosti 2009

Wataliban wazidisha hujuma kabla ya uchaguzi mkuu

https://p.dw.com/p/J79N
Vikosi vya jeshi la Ujerumani huko KundusPicha: AP

Wataliban wamehujumu majengo kadhaa ya serikali hii leo,umbali wa kilomita 50 kusini mwa mji mkuu Kabul huku mapigano yakiendelea dhidi ya vikosi vya usalama.Askari polisi mmoja ameuwawa.

Mashambulio hayo ambayo waasi wanadai dhamana,yamesadif siku kumi tuu kabla ya uchaguzi wa rais, wa pili katika historia ya nchi hiyo,pamoja pia na ule wa mikoa.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya mkoa,Din Mohammed Darwish,waasi,waliojifungia katika majengo ya karibu na hapo wamevurumisha makombora na risasi dhidi ya ofisi ya Gavana na makao makuu ya polisi huko Pul-i-Alam,kilomita 50 kusini mwa mji mkuu Kaboul.

"Waasi wamejificha ndani ya majengo mawili ya ghorofa wakizungukwa na vikosi vya usalama na kutupiana nao risasi."Amesema hayo Din Mohammed Darwish wakati wa mahojiano pamoja na shirika la habari la Ufaransa AFP.Milio ya risasi ilikua ikisikika wakati wa mahojiano hayo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani,Zemarai Bashary amesema kwa upande wake kwamba askari polisi mmoja ameuwawa,akithibitisha ripoti kwamba vikosi vya usalama vya Afghanistan na vikosi vya kimataifa vimewazingira waasi."Watakamatwa tuu au watauliwa" amesema.

Vikosi vya kimataifa vya Nato na vile vinavyoongozwa na Marekani havijathibitisha lakini ripoti za kushiriki kwao mapiganoni.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Zemarai Bachary amekanusha ripoti za wataliban wanaodai kwamba watu waliojifunga miripuko wameingia katika ofisi ya gavana.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya mkoa , makombora ya wataliban yaliopiga ndani ya ofisi ya gavana na makao makuu ya polisi,hayakusababisha hasara yoyote ya maisha.

Msemaji wa wataliban-Zahibullah Mujahed akitangaza kuhusika kwao na mashambulio hayo amedai watu 21 wameuwawa.

Mashambulio haya ya leo yamejiri katika wakati ambapo vikosi vya usalama vya Afghanistan na washirika wao wa kimataifa wamekua wakijiandaa kudhamini usalama kwaajili ya uchaguzi mkuu wa Agosti 20 ijayo.

Schweiz Afghanistan Wirtschaft Weltwirtschaftsforum in Davos Hamid Karsai
Rais Hamid Karsai wa AfghanistanPicha: AP

Wataliban wanaofanya mashambulio ya kikatili tangu walipotimuliwa madarakani na vikosi shirika vinavyoongozwa na Marekani mwishoni mwa mwaka 2001,wamewatolea mwito waafghanistan waususie uchaguzi huo.

Kuna wanaohofia kwamba mashambulio hayo yanaweza kuwatia hofu wapiga kura wasiteremke kwa wingi vituoni na kwa namna hiyo kuyatia ila matukio ya uchaguzi yanayopewa umuhimu mkubwa na jumuia ya kimataifa.

Mwandishi:Oummilkheir Hamidou