1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio ya mabomu katika Jakarta

Miraji Othman17 Julai 2009

Tena mashambulio ya kigaidi Indonesia?

https://p.dw.com/p/Iroh
Maofisa wa polisi wanafanya upelelezi katika Hoteli ya Marriott, mjini Jakarta, baada ya kushambuliwa kwa bomu.Picha: AP

Katika mashambulio mawili ya mabomu kwenye hoteli mbili za kifahari katika mji mkuu wa Jakarta, huko Indonesia, hapo jana, zaidi ya watu wanane walikufa na madarzeni wengine walijeruhiwa vibaya. Mashambulio hayo yanakumbusha mashambulio makubwa yaliofanywa katika kisiwa cha utalii cha Bali, katika nchi hiyo hiyo ya Indonesia, hapo mwaka 2000, ambapo zaidi ya watu 200 waliuwawa.
Risala ni ya kusikitisha. Licha ya kuchukuliwa hatua zote za kulinda usalama na pia kuwa na siasa madhubuti ya kupambana na ugaidi, wauaji, kwa mara nyingine tena, wameweza kushambulia kwenye moyo wa Indonesia. Shambulio hilo la Jakarta ni pigo kubwa kwa rais wa Indonesia, Susilo Bambang Yudhoyono, aliyechaguliwa upya hivi karibuni. Katika miaka ya karibuni mambo yalikuwa tulivu, Tukizungumzia juu ya tawi la mtandao wa al-Kaida, ambalo ni jumuiya ya kigaidi ya Jamiah Islamiah, ambayo inafikiriwa kuwa ndio ilio nyuma ya mashambulio hayo ya jana.

Hata hivyo, majeshi ya usalama ya Indonesia yalipata mafanikio madogo dhidi ya washabiki wa jumuiya hiyo, licha ya kwamba kunyongwa kwa wale waliofanya mashambulio ya Bali kuligonga vichwa vya habari. Licha ya kwamba duniani kote idadi ya mashambulio ya kigaidi imeongezeka, hata hivyo, Indonesia, iliobakia muda mrefu katika mshtuko wa shambulio kubwa la mabomu la huko Bali mwaka 2002, ilionekana imeweza kulidhibiti tatizo hilo la ugaidi.

Lakini sasa mtu inafaa aachane na kasumba hiyo. Vizuwizi vya usalama, ambavyo mtu kwa kawaida hukabiliana navyo katika hoteli zote kubwa za kifahari huko Indonesia, havijaweza kuzuwia shambulio hili la jana. Na inaonesha mtandao wa magaidi unaweza kufanya hujuma za wakati mmoja katika maeneo mengi ya mji mkuu wa Indonesia.

Kulifanywa shambulio la kigaidi huko Bali, lengine katika ubalozi wa Australia nchini humo na wakati mmoja katika hoteli ya Marriot mjini Jakarta. Kama ilivyokuwa hapo kabla, mara hii mashambulio hayo yaliwalenga pia raia wa kigeni. Hoteli zote mbili zilizoshambuliwa jana zinajulikana kwa kuwa na wageni wa kutoka mataifa mbalimbali. Lakini wanaoathirika katika mashambulio hayo wengi ni raia wa Indonesia, watu ambao wanakuwa hawako mbali na mahala panaposhambuliwa.

Ni katika muda wa karibuni ambapo biashara ya utalii imeanza kupata afuweni baada ya mashambulio ya Bali. Na pindi sasa wageni wataonywa wasifanye safari hadi Indonesia, basi mkondo wa kupanda juu biashara hiyo utazuilika. Ikiwa wawekezaji watatishiwa kutokana na ugaidi huu, ni suala la kungojea na kuona.

Sura za hoteli za Jakarta zilizoharibiwa kwa mabomu zitaichafua tena sura ya nchi hiyo ilio na idadi kubwa kabisa ya Waislamu duniani. Ni wazi kwamba, kama walivofanya hapo kabla, wananchi wa Indonesia watadhihirisha kwamba siasa za itikadi kali za kidini hazina nafasi katika nchi yao. Pia vyama vya kidini haviungwi mkono na watu wengi, na havina nafasi katika chaguzi.

Indonesia sio tuu ni nchi yenye Waislamu wengi hivi sasa, lakini nchi hiyo pia ni yenye ustahamilivu mkubwa kabisa miongoni mwa nchi za Kiislamu. Inasikitisha zaidi kwamba nchi hiyo sasa inagonga vichwa vya habari za dunia kama mahala pa shughuli za kigaidi.

Malengo ya wauwaji hao kwa sasa yanaweza tu kushukiwa. Wazi ni kwamba wauwaji hao wameweza kuiletea hasara nchi hiyo. Lakini ikiwa wanataraji kwamba, kupitia mashambulio haya ya ghafla, wanaweza kupata wafuasi wengi, basi watavunjika moyo huko Indonesia.

Kinyume na hivyo: Indonesia itaitia makali siasa yake ya kupambana na ugaidi, na Rais Yudhoyono anaweza kutegemea kuungwa mkono na wananchi ambao tangu mashambulio ya Bali wamedhihirisha kwamba wamechoshwa na siasa za matumizi ya nguvu na itikadi kali.