1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio zaidi nchini Afghanistan-Watu 12 wauawa leo

Jane Nyingi/ AFPE..Picha AFP28 Oktoba 2009

Watu kumi na wawili wakiwemo wafanyikazi sita wa Umoja wa Mataifa wameuawa nchini Afghanistan kufuatia mlipuko katika hoteli mmoja mjini Kabul.

https://p.dw.com/p/KHeH
Wanajeshi wa Nato wakishika doria mjini KabulPicha: AP

Watu waliokuwa wamejihami kwa silaha waliivamia hoteli hiyo inayomilikiwa na wageni hali iliyosababisha mapiganao makali ya risasi. Tukio hilo limeibua maswali mengi kuhusu hali ya usalama wakati wa duru ya pili ya uchaguzi wa urais mwezi ujao.

Kundi la Taliban limekiri kuhusika katika shambulio hilo mjini Kabul lilosababisha pia vifo vya maafisa wawili wa usalama raia wa Afghanistan na washambuliaji watatu. Akizungumza kwa njia ya simu katika eneo lisilojulikana msemaji wa kundi la Taliban Zabiullah Mujahid, alisema waliganaji watano wa Taliban waliokuwa wamejihami kwa silaha walivamia hoteli hiyo, wakiwalenga wafanyikazi wa shirika la Umoja wa mataifa.

Afisa mmoja wa polisi aliyekuwa katika eneo la tukio aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa wanashuku waliotekeleza shambulio hilo ni raia wa Pakistan. Wengi wa wapiganji wa Taliban nchini Aghanistan wametafuta hifadhi katika nchi jirani ya Pakistan au wao wenyewe ni wapakistan.

Mwishoni mwa juma lilopita wapiganaji hao walikuwa wametishia kulenga Wafghanistan na wafanyikazi wa kigeni wanaojihusisha na matayarisho ya duru ya pili ya uchaguzi huo wa rais utakaofanyika November 7. Mujahid amesema shambulio hilo mjini Kabul ndio mwanzo tu wa mengine yatakayofwata. Wapiganaji hao pia wamewaonya Wafghan kutoshiriki katika uchaguzi huo la sivyo washambuliwe.

Juhudi za kurejesha hali ya utulivu nchini Afghanistan zimekabiliwa na chanagamoto nyingi kutokana na hali mbaya ya kisiasa nchini humo, kufuatia uchanguzi wa Agosti mwaka huu ambao ulikabiliwa na wizi wa kura ili kumrejesha madarakani rais Hamid Karzai .

Mapigano nchini humo yameongezeka .Hapo jana jumanne wanajeshi wanane wa Marekani waliuawa katika shambulio kusini mwa Afghanistan. Marekani ina thuluthi tatu ya wanajeshi wa kulinda amani wa shirika la kujihami la Nato walioko nchini humo.Wafuasi wa rais Karzai wamesema duru ya pili ya uchaguzi huo lazima yafanyike hata kama mpinzani wake wa karibu Abdullah Abdullah ataamua kujiondoa.

Wiki iliyopita, Karzai alikubali kufanyika kwa duru hiyo ya pili ya uchaguzi wa urais kufuatia shinikizo kubwa la kimatiafa baada ya uchunguzi uliofanywa na Umoja wa mataifa kubaini kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa na wizi wa kura katika uchaguzi huo

Chini ya mkakati mpya wa Marekani nchini Afghanistan,rais Barack Obama anatazamiwa kukutana Ijumaa wiki hii na Admirali Mike Mullen mwenyekiti wa uongozi wa vikosi vya majeshi ya Marekani.

Wakati huo huo roketi mbili zimerushwa hii leo mjini Kabul moja ikilienga hoteli ya kifahari ya Serena ambayo iko karibu na makaazi ya rais.Hivi sasa polisi wamezingira hoteli hiyo,ambayo ilishamgbuliwa na mplipuaji wa kujitoa mhanga Januari mwaka jana na kuwauwa watu sita.

Mwandishi:Jane Nyingi/DPAE

Mhariri:Abdul-Rahman.