1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya maguruneti yameua polisi 16 China

P.Martin4 Agosti 2008

Ikiwa ni siku chache tu kabla ya kufunguliwa Michezo ya Olimpiki katika mji mkuu wa China Beijing,shambulizi dhidi ya kituo cha ukaguzi cha mpakani,kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo limeua polisi 16.

https://p.dw.com/p/EqC4
Security personnel stand guard outside the International Broadcasting Centre (IBC) at the Olympic Green in Beijing, China which opened 08 July 2008, one month prior to the opening ceremony of the 29th Olympiad. The centre along with the adjoining Main Press Centre will host over 21,000 journalists from around the world during the upcoming Beijing Olympics which commence 08 August. EPA/ADRIAN BRADSHAW (zu dpa 0157 vom 08.07.2008) +++(c) dpa - Report+++
Vikosi vya usalama vikilinda kituo cha matangazo ya kimataifa kilichofunguliwa Beijing kwa Michezo ya Olimipiki.Picha: picture-alliance/ dpa

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la China Xinhua, washambulizi wawili walibamiza lori lao kwenye kituo cha polisi wa mpakani katika Wilaya ya Xinjiang na wakarusha maguruneti na kuwapiga visu polisi.Mripuko wa maguruneti uliua polisi 16 na kujeruhi pia 16 wengine.Washambulizi wote wawili wamekamatwa lakini kwa hivi sasa haijulikani ni kundi gani hasa lililohusika.

Shambulizi hilo limetokea katika mji wa Kashgar wilayani Xinjiang,ambako huishi watu wa kabila la Uighur ambao ni Waislamu wapatao kama milioni nane.Wakaazi hao wanapinga utawala wa China na ule ushawishi wa Wachina wa kabila la Han,unaozidi katika eneo hilo la utajiri wa gesi asilia.

Wenyeji wa wilaya hiyo wanalalamika kuwa serikali ya Beijing inawankandamizwa kitamaduni na kisiasa huku baadhi ya makundi ya Wauighur yakitaka uhuru wa wilaya hiyo.Kwa mujibu wa China,wanamgambo wamejiunga na makundi ya kigaidi kama vile al-Qaeda na Hizb ut-Tahrir.

Vyombo vya habari nchini China vimesema,polisii ilipata fununu kuwa Chama cha Kiislamu cha Turkestan ya Mashariki kimepanga kufanya mashambulizi ya kigaidi kabla ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki.Shambulizi la hii leo kwa kweli,ni pigo kubwa kwani hatua za kulinda usalama hasa wilayani Xinjiang zimeimarishwa kwa hali ambayo haijawahi kutokea.Hatua hizo za usalama hasa zimewalenga Waislamu wa Uighur.

Kwa maoni ya China,wanamgambo wanaogombea uhuru wa Turkestan ya Mashariki ni miongoni mwa vitisho vikubwa.Serikali imesema,imefanikiwa kuzuia mipango ya magaidi waliotaka kuishambulia Michezo ya Olimpiki.Vile vile katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu,katika wilaya ya Xinjiang polisi waliwawatia mbaroni watu darzeni kadhaa kwa sababu ya kupanga kuichafua Michezo ya Beijing.

Lakini wanaharakati wanaotetea haki za binadamu na hata Wauighur wanaoishi uhamishoni wanasema, serikali ya China inatia chumvi kuhusu vitisho vya machafuko katika wilaya ya Xinjiang. Wanasema,kinyume ni kuwa China ndio iliyochochea machafuko kwa kupeleka Wachina zaidi wa kabila la Han katika eneo la Waiughir.Kwani sasa,idadi ya Wauighur si hata nusu ya wakaazi wapatao milioni 20 katika Wilaya ya Xinjiang kaskazini-magharibi ya China.