1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Trump dhidi ya Ujerumani yazusha hofu

Iddi Ssessanga
26 Mei 2017

Rais wa Marekani Donald Trump ameanzisha mashambulizi dhidi ya biashara ya mauzo ya magari ya Ujerumani nchini Marekani, katika ishara ya hivi karibuni ya mzozo wa biashara katika kanda ya atlantiki.

https://p.dw.com/p/2deNt
G7 Treffen in Taormina Sizilien Italien Merkel, Trump
Picha: Getty Images/AFP/P. Wojazer

Akizungumza baada ya vyombo vya habari vya Ujerumani kumripoti rais wa Marekani akiwaelezea Wajerumani kuwa wabaya, Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker alijaribu kupunguza uzito wa mgogoro huo wa karibuni zaidi tangu alipoingia madarakani akitanguliza sera yake ya Marekani kwanza.

Akipendekeza kuwa matamshi yaliyoelekezwa kwa Trump yalikuwa yamepotoshwa, Juncker alithibitisha kwamba Trump alizungumzia ziada kubwa ya biashara ya Ujerumani na Marekani katika sekta ya magari wakati wa mazungumzo mjini Brussels siku ya Alhamisi. Akijibu swali la mwandishi wa habari alieuliza iwapo ni kweli Trump alisema Wajerumani ni wabaya, Juncker alisema katika mkutano wa G7 nchini Italia uliohudhuriwa na Trump na Kansela wa Ujerumani angela Merkel kwamba suala hilo limetiliwa chumvi.

"Sitaki kuzungumzia lakini nalaazimika kulizungumzia hili kwa sababu tulikuwa na mkutano na Rais Trump ambao ulikuwa wa kirafiki sana na wa manufaa. Siyo kweli kwamba rais alichukuwa msimamo wa kishari kuhusu ziada ya biashara ya Ujerumani. Nadhani kiukweli, na kwa mara ya kwanza ni kweli, kwamba huu ni mfumo halisi wa tafisiri."

G7 Treffen in Taormina Sizilien Italien
Viongozi wakuu wa kundi la mataifa saba yalioendelea zaidi kiviwanda duniani G7 wakiwa katika mkutano wao wa kilele mjini Taormina nchini Italia, Mei 26,2017.Picha: Reuters/J. Ernst

Ujumbe ulifikishwa lakini si kwa ushari

Mshauri wa kiuchumi wa Trump Gary Cohn pia alisisitiza kuwa majibizano hayo yalikuwa ya kirafiki lakini kwamba suala muhimu kwa utawala mpya wa Marekani lilikuwa limewekwa mezani. Cohn alieleza kuwa Trump alisema Wajerumani ni wabaya kwenye biashara lakini binafsi hana tatizo na Wajerumani.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Ujerumani, Trump alilamika vikali kuhusu kampuni mfano wa Volkswagen, BMW na Mercedes kuuza mamilioni ya magari nchini Marekani na kuapa kukomesha mauzo hayo. Bila kujali ukweli hasa ni upi, suala hilo halikuwazuwia Trump na Merkel kufurahia wakati wao pamoja mwanzoni mwa mkutano wa G7, walipoonekana wakicheka wakiwa pamoja na waziri mkuu wa Uingereza Theresa May na rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk.

Wasaidizi wa Juncker walishutumiwa mwezi uliopita kwa kuvujisha maelezo ya mkutano wa chakula cha jioni alioufanya na May kuhusu Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya. Uvujishaji huo ulivifikia vyombo vya habari vya Ujerumani na kumlaazimu Tusk kuonya kwamba kukosekana kwa faragha kutayafanya mazungumzo ya Brexit kuwa magumu. Alitoa onyo sawa jana Ijumaa.

Wasiwasi miongoni mwa wanachama wa G7

Suala la magari ya Ujerumani liliripuka mnamo wakati wasiwsi umetanda miongoni mwa washirika wa Marekanio katika kundi la G7 kwamba sera ya Trump ya Amerika kwanza huenda ikasababisha hatua za kujihami ambazo zinaweza kurudisha nyuma miongo kadhaa ya uhuru wa kibiashara miongoni mwa mataifa yalioendelea zaidi duniani.

USA VW Passat
Kiwanda cha kampuni ya Volkswagen mjini Los Angeles Marekani. Rais Donald Trump ametishia kuzuwia uuzaji wa magari ya Kijerumani nchini Marekani.Picha: picture-alliance/dpa/Foto: Friso Gentsch/Volkswagen

Wakati wa kampeni zake za uchaguzi, Trump alizituhumu China, Ujerumani na matifa mengine kwa kuendesha ziada ya biashara na Marekani kwa kuharibu nafasi za ajira na maendelea ya Wamarekani wa kawaida kwa msaada wa sarafu zilizochezewa.

Tangu kuchaguliwa kwake bado hajatekeleza hatua zozote muhimu za kujihami na Umoja wa Ulaya umeyatafsiri makubaliano ya kufungua biashara kati ya Washington na China, kama ishara kwamba unyumbulifu na utashi vina uwezekano mkubwa wa kuongoza sera ya biashara ya Marekani.

Kilio hata ndani ya Ulaya

Ziada ya biashara ya Ujerumani iliofikia rekodi ya euro bilioni 253 mwaka 2016, pia imekuwa suala linalozusha ubishani hata ndani ya Ulaya yenyewe, ambapo washirika wa Berlin wanaishinikiza kufanya zaidi kukuza mahitaji ya ndani.

Ujerumani imejibu ukosoaji ikiielezea ziada yake kama matokeo ya bidhaa zake zenye ushindani, hasa magari, na sera huru ya  rahisi ya benki kuu ya Ulaya, ambayo imepelekea kushuka kwa thamani ya euro na hivyo kuzifanya bidhaa za Ujerumani kuvutia zaidi nje.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtreafpe

Mhariri: Josephat Charo