1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yaelekezwa jimbo la Aleppo

Isaac Gamba13 Aprili 2016

Utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Syria ulikuwa hatihati kuvunjika kufuatia kuibuka upya kwa mapigano hususani katika jimbo la kaskazini la Aleppo

https://p.dw.com/p/1IU7u
Picha: picture alliance/abaca

Mapigano haya yanakuja huku mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Syria Steffan de Mistura ambaye alikuwa nchini Iran kwa ajili ya mazungumzo na wale wanaounga mkono utawala wa rais Bashar al-Assad wa Syria akisema mazungumzo hayo ya amani yatakuwa ya umuhimu mkubwa.

Mazungumzo ya amani ya wiki hii yatakuwa ni ya pili tangu kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya upande wa serikali ya Syria na makundi ya waasi yaliyoridhiwa pia na mataifa ya Urusi na Marekani ambayo utekelezaji wake ulianza tangu Februari 17, mwaka huu.

Hatua hii imezidi kuongeza matumaini katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo wa Syria uliodumu kwa muda wa miaka mitano sasa na kusababisha vifo vya kiasi ya watu 270,000.

Mashambulizi yalengwa katika mji wa Aleppo

Hata hivyo mashambulizi ya hivi karibuni yaliyolengwa zaidi katika jimbo la Aleppo liliko mpakani na Uturuki yanatishia utekelezaji wa hatua hiyo ya kusitisha mapigano.

Mapambano Kati ya jeshi huru la Syria na kundi la IS Karibu na mpaka wa Uturuki
Mapambano Kati ya jeshi huru la Syria na kundi la IS Karibu na mpaka wa UturukiPicha: picture-alliance/AA/I. Mazi

Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria limesema majeshi tiifu kwa serikali ya nchi hiyo yamekuwa yakisonga mbele kuelekea katika mji wa Al-Eis unaodhibitiwa na wapiganaji wa kundi la Al-Nusra Front na majeshi washirika lenye mafungamano na kundi la itikadi kali la Al-Qaeda.

Makundi ya itikadi kali kama vile ya Al-Nusra na lile la Dola la Kiislamu hayahusiani na makubaliano yaliyofikiwa katika hatua ya kusitisha mapigano nchini humo lakini katika maeneo mengine wanamgambo wa kundi la Al-Qaeda wanaonekana kuwa washirika na makundi ya waasi ambao walitia saini makubaliano hayo ya kusitisha mapigano.

Majeshi ya serikali ya Syria yanayoungwa mkono na Urusi yalifanya mashambulizi katika mji wa Aleppo wakati mazungumzo ya awali yaliyofanyika mwishoni mwa mwezi Januari yalipokwama.

Nchi za Magharibi zililaumu hatu hiyo ya majeshi ya serikali ya Syria ya kuzidisha mapambano na hivyo kuhatarisha mafanikio ya kupatikana kwa suluhu ya mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo.

Marekani yaonya kushambuliwa kundi la Al-Nusra

wapiganaji wa kundi la Al-Nusra Front
wapiganaji wa kundi la Al-Nusra FrontPicha: Getty Images/AFP/O.H. Kadour

Marekani imeonya kuwa mashambulizi dhidi ya kundi la Al-Nusra katika mji wa Aleppo yanaweza yakaleta athari pia kwa makundi ya waasi wenye msimamo wa wastani na hivyo kusababisha kusambaratika kwa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano hali itakayozorotesha mazungumzo ya amani.

Shirika la Human Rights Watch nalo pia limeonya juu ya kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya raia kuwa kunaweza pia kusababisha kuvunjika kwa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano.

Kuibuka upya kwa mapigano haya hasa katika mji wa Aleppo kunakuja mnamo wakati upande wa serikali ya Syria na ule wa makundi ya waasi ukikutana mjini Geneva siku ya Jumatano kuendelea na mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa Syria huku suala la Rais Bashar Assad wa Syria likiwa bado ni kikwazo.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE.

Mhariri: Iddi Ssessanga