1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yatishia mpango wa kusitisha mapigano Syria

2 Januari 2017

Urusi na Uturuki zimefanya mashambulizi ya anga dhidi ya ngome za kundi linalojiita Dola la Kiislamu ndani ya Syria na jeshi la Syria limewashambulia waasi katika hali inayouweka mashakani mpango wa kusitisha mapigano.

https://p.dw.com/p/2V7um
Syrien Assad Regime verletzt Waffenruhe in Aleppo
Jeshi la serikali ya Syria limekuwa likiendelea kuzilenga ngome za waasiPicha: picture alliance/dpa/AA/A. al Ahmed

Mashambulizi ya Uturuki kwa kutumia ndege za kivita na mizinga vimewauwa wapiganaji 22 wa kundi la IS ndani ya Syria, huku yale ya Urusi yakijikita zaidi katika mji wa al-Bab unaodhibitiwa na kundi hilo la kijihadi. Jeshi la serikali limesema pia katika taarifa yake, kuwa mashambulizi hayo ya Urusi yamekiharibu kituo cha Dola la Kiislamu katika eneo la Dayr Kak umbali wa km 8 kutoka mji wa al-Bab.

Hayo yanaarifiwa wakati Shirika linalochunguza haki za binadamu nchini Syria, likiripoti kuwepo mashambulizi ya jeshi la serikali ya Syria dhidi ya waasi katika bonde lililopo karibu ya mji mkuu, Damascus, baada ya siku mbili za utulivu uliotokana na kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha uhasama.

Jumamosi iliyopita, waasi walionya kuwa wangejiondoa katika makubaliano hayo iwapo serikali itaendelea kuwashambulia, na kuitaka Urusi ambayo ni mshirika mkuu wa serikali ya Rais Bashar al-Assad kuishinikiza serikali hiyo kusimamisha hujuma zake ifikapo saa nane mchana. Mashambulizi ya anga yalisitishwa kabla ya muda huo, lakini makabiliano ya aina nyingine yaliendelea jana Jumapili.

Raia wahamia katika maeneo ya serikali

Syrien Damaskus Wasserkrise
Raia wamekuwa wakihamia katika maeneo yanayodhibitiwa na serikaliPicha: picture-alliance/dpa/Y. Badawi

Mashambulizi ya serikali yaliyalenga maeneo ya Wadi Barada ambalo lilishambuliwa vikali na serikali na washirika wake zaidi ya wiki moja iliyopita, hii ikiwa ni kwa mujibu wa msemaji wa kundi la Jaish al-Nasr aliyezungumza na shirika la uchunguzi lenye makao yake nchini Uingereza.

Msemaji huyo Mohammed Rasheed alisema serikali ya Rais Assad na washirika wake wa kishia waliendesha mashambulizi yao kutoka vilima vilivyo karibu ya Wadi Barada.

Duru za shirika la uchunguzi wa haki za binadamu na za vyombo vya habari vya serikali, zimearifu kuwa raia walihama kutoka Wadi Barada na kukimbilia katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa serikali. Aidha, duru hizo zimesema jeshi la serikali limesonga mbele katika sehemu za Ghouta Mashariki mwa Damascus, na kuyateka mashamba kumi.

Ujerumani yatilia shaka

Frankreich Frank-Walter Steinmeier in Paris
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Frank-Walter SteinmeierPicha: Reuters/B. Tessier

Afisa mwingine wa upinzani amesema mashambulizi madogo madogo hayawezi kuyavunja makubaliano ya kusitisha mapigano, lakini yale ya anga yatachukuliwa kama ukiukaji mkubwa. Hata hivyo wizara ya ulinzi ya Urusi imewashutumu waasi kuwa wao ndio waliofanya uchokozi mara kadhaa.

Makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Urusi na Uturuki na yaliungwa mkono katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, yanadhihirisha kuongezeka kwa ushawishi wa kidiplomasia wa Urusi, baada ya mashambulizi ya anga ya muda mrefu dhidi ya waasi, ambayo yamemwezesha Rais Assad kuukamata tena mji wa Aleppo mwezi uliopita.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ametilia shaka iwapo makubaliano hayo yatafanikiwa, akisema zinahitajika hatua nyingine zaidi ya kusitisha uhasama wa kijeshi. Hata hivyo amesifu kuendelea kuheshimiwa kwa makubaliano hayo, akisema ni habari njema kwa watu wa Syria.

Ushindi huo wa Aleppo umeiweka serikali ya Damascus katika nafasi nzuri, kuelekea katika mazungumzo ya kutafuta amani yatakayaofanyika nchini Kazakhstan baadaye mwezi huu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre,afpe
Mhariri: Grace Patricia Kabogo