1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashindano ya riadha ya dunia: Berlin.

18 Agosti 2009

Wakenya wasubiri kwa hamu mbiko za mita 3000 kuruka viunzi, wanaume.

https://p.dw.com/p/JDgE
Pamela Jelimo akosa kufuzu kwa mbio za mita 800.Picha: AP

Baada ya kutia kibindoni medali moja ya dhahabu na mbili za shaba, Kenya leo wameweka matumaini ya kupata medali zingine tatu- katika mashindano ya mbio za mita elfu tatu kuruka viunzi. Kipruno Richard Kemboi na Brimin Kipruto ndio watapeperusha bendera ya Kenya katika mbio hizo ambazo wamezitawala kwa muda mrefu- na wameahidi kuendeleza umahiri wao, mjini Berlin katika mashindano yanayoendelea ya riadha ulimwenguni.

Wamarekani pia watakuwa wanajaribu kuwapiku Wajamaica katika mbio za mita 400 kwa kina dada.

Pale bingwa wa olimpiki, Brimin Kipruto na Kipruno Richard Kemboi watakapoingia uwanjani kutetea taji la mbio za mita 3000 kuruka viunzi- Wakenya wengi roho zitakuwa juu juu- je tutaendelea kutamba?

Tayari mjini Berlin idadi ya medali za dhahabu kwa Kenya imeingia dosari- kufuatia kuondoka jana katika mashindano hayo kwa bingwa wa olimpiki katika mita 800 kwa kina dada Pamela Jelimo.

Hivyo uwanja sasa utakuwa kwa Kemboi na Kipruto. Na ingawa mazoea imekuwa Kenya kutwaa namba 1-2-3 bado kuna upinzani kutoka kwa Wakenya waliohamia nchi za Kiarabu- Mubarak Taher kutoka Bahrain atakuwa anawahemea wakenya mgongoni.

Lakini Kipruto Kemboi anasema wako tayari na wamejitayarisha kama timu, hivyo watu wasubiri medali.

Milka Chemos Cheywa aliyeondoka na medali ya shaba jana katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi kwa kina dada anasema alikuwa amepania kunyakua dhahabu lakini jana haikuwa siku yake.

Mhispania Dominiquez ndiye aliyeshinda dhahabu.

Matumaini ya Kenya katika mita 800 za kina dada yote yaliwekwa mabegani mwa bingwa olimpiki Pamela Jelimo- lakini uwanja wa Berlin hautashuhudia umahiri wa Jelimo mwaka huu- kwani alikosa kufuzu alipojiondoa baada ya mita 400. Wakenya walikufa moyo, Jelimo anasema alikufa moyo zaidi.


'' Nilitaka sana kuiwakilisha Kenya, nilisikitika sana sikuweza. Nilianza vizuri lakini baada ya kukimbia mita 400 nikaanza kusikia uchungu katika goti langu la kushoto. Ilibidi niage mashindano, lau sivyo ningepata jeraha baya zaidi.''


Kibarua sasa kimo na bingwa wa dunia Janeth Jepkosgei anayejulikana kama Eldoret Express. Ingawa Janeth naye jana aliingia chupuchupu katika fainali hizo.

Msisimko mwingine jioni hii mjini Berlin ni mbio za mita 400 za kina dada. Bingwa wa olimpiki Nwachuku kutoka Uingereza atakuwa anajibidisha kuzima makali ya Sherika William kutoka Jamaica na Sanya Richard kutoka Marekani anayepigiwa upatu kuwa yupo katika nafasi nzuri ya kutwaa kuponyoka na medali ya dhahabu. Hadi sasa mbio za mita 200 na 100 za kina dada zimenyakuliwa na Wajamaica.

Mbio za mita 400 kwa wanaume kuruka viunzi pia zinafanyika usiku huu. Angelo Taylor kutoka Marekani ambaye pia ni bingwa wa Olimpiki ataongoza wenzake wawili kutoka Marekani na Muingereza mmoja kujikatia nani ndiye bora duniani.

Mwandishi: Munira Muhammad/ape

Mhariri: Abdul-Rahman