1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yaitishwa dhidi ya ziara ya Mohammed bin Salman

26 Novemba 2018

Muungano wa wanahabari Tunisia pamoja na mashirika ya kijamii leo wameitisha maandamano dhidi ya ziara ya Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin Salman, kufuatia mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi.

https://p.dw.com/p/38vbB
Tunesien Proteste gegen Besuch Saudi Kronprinz Mohammed bin Salman
Bango lilitundikwa nje ya ofisi ya Muungano wa Wanahabari katika mji wa Tunis yenye maandishi,'Bin Salman hakaribishwi Tunisia,ardhi ya mapinduzi.'Picha: Getty Images/AFP/F. Belaid

Rais wa Tunisia Beji Caid el Sebsi amesema kiongozi huyo wa Saudi atazuru taifa hilo kwa saa kadhaa kesho Jumanne ikiwa mojawapo ya ziara yake ya kimaeneo, bila kutoa maelezo zaidi kuhusiana na ratiba yake. Maandamano hayo yamepangwa kufanyika jioni ya leo katikati mwa mji wa Tunis na mji wa Sfax.

Saudi Arabia imekuwa ikipokea ukosoaji mkubwa wa kimataifa kufuatia mauaji ya Khashoggi mjini Istanbul tarehe 2 Oktoba mwaka huu. Kwenye barua kwa Ofisi ya Rais nchini Tunisa, muungano wa wanahabari nchini humo umesema kwamba ziara ya Mohammed Bin Salman inatishia usalama na Amani pamoja na ulimwengu, vile vile tishio kwa uhuru wa kujieleza. Aidha wanasema inakiuka kanuni ya mapinduzi.

Uchunguzi wa kutafuta mabaki ya mwili wa Khashoggi

Türkei Fall Khashoggi - Trauergebete
Picha: picture-alliance/dpa/AP/E. Gurel

Hayo yakijiri, maafisa wa polisi wa Uturuki pamoja na mbwa wa kunusa wamefanya ukaguzi katika majengo mawili ya kifahari Magharibikaskazini mwa Uturuki leo, ikiwa mwendelezo wa uchunguzi wa mauaji ya Jamal Khashoggi. Maafisa wanaoendeleza uchunguzi huo wamesema kwamba kisima kilichoko kwenye mojawapo ya majengo hayo ndiho kilichokuwa kikilengwa, huku taarifa katika vyombo vya habari vya Uturuki vikisema kuwa walikuwa wakitafuta mabaki ya mwili wake.

Gazeti la Hurriyet limesema moja wapo ya majengo hayo mawili ya kifahari yanamilikiwa na mfanyabiashara mmoja wa Saudi Arabia lakini hawakumtaja jina. Gavana wa eneo la Yalova Mummaer Erol amesema kwamba tangazo kuhusiana na msako unaoendelea litatolewa na mkuu wa mashtaka anayeongoza uchunguzi wa taifa la Uturuki kuhusiana na mauaji hayo.

Medien Türkei Istanbul Zeitungskiosk
Picha: Getty Images/C. McGrath

Uturuki imesisitiza kwamba maagizo ya kuuawa kwa Khashoggi yalitolewa na mmoja wa wakuu wa serikali ya Saudi,lakini sio Mohammed bin Salman. Salman alianza ziara yake kufuatia ombi la baba yake Mfalme Salman, ikiwa ni kulingana na Idara ya Habari ya Saudi,ambayo ilisema atazuru mataifa ya  Kiarabu. Mrithi huyo wa Ufalme atawasili mjini Cairo Misri kufanya mazungumzo na Rais Abdel Fatah al-Sisi. Anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa G20 nchini Argentina wiki ijayo.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman