1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo haijawaadhibu wakiukaji wa haki za binadamu

Tatu Karema
2 Oktoba 2020

Mashirika ya kutetea haki ya binadamu ya Amnesty International na Human Rights watch yasema Mamlaka nchini Congo na UN hazijafanya Vya kutosha kuchukulia hatua wakiukaji wa haki za binadamu na kutoa haki kwa waathiriwa.

https://p.dw.com/p/3jKSY
Präsident des Kongos: Felix Tshisekedi
Picha: picture-alliance/AA/M. Hailu

Ripoti hiyo ilirekodi zaidi ya matukio 600 ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu za kimataifa na sheria za kibinadamu uliofanywa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kati ya Machi 1993 na Juni 2003.

Mkurugenzi wa shirika la Amnesty International katika kanda ya Afrika Mashariki na Kusini Deprose Muchena, amesema kuwa kushindwa kutambua na kuweka utaratibu wa kutosha wa kutoa haki na fidia kumeacha maelfu ya waathiriwa na familia zao bila usaidizi na matokeo yake ni kwamba hali ya uvunjaji sheria bila hofu ya kuchukuliwa hatua inaendelea kukithiri nchini humo na maeneo mengine ya kanda hiyo na kusababisha mauaji ya mara kwa mara na uhalifu mwingine mbaya.

Shirika hilo pia limesema kuwa rais Felix Tshisekedi anapaswa kutoa kipaumbele kushugulikia hali ya uvunjaji sheria bila ya hofu ya kuchukuliwa hatua na kuchukuwa hatua madhubuti dhidi ya wale waliohusika katika ukiukaji wa sasa na uliopita wa haki za binadamu.

Michel Luntumbue GRIP
Michel Luntumbue- Mtafiti mwandamizi GRIPPicha: Wendy Bashi

Katika mahojiano na DW, Michel Luntumbue, mtafiti mwandamizi wa shirika linalofanya utafiti kuhusu masuala ya usalama, GRIP, lenye makao yake mjini Brussels, Ubelgiji, alizungumzia kipindi cha mpito nchini Congo ambapo mshindi wa zamani wa tuzo ya amani ya Nobel Dr Dennis Mukwege amewahi kupendekeza kuundwa kwa mahakama maalumu itakayoshughulikia makosa ya ukiukaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa, kama ilivyoanishiswha pia katika ripoti ya Umoja wa Mataifa.

Changamoto za kuanzishwa kwa mahakama maalumu 

Luntumbue anasema bado kuna changamoto kubwa katika kuanzishwa kwa mahakama hiyo. Amesema kwa sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaendesha mchakato wa mageuzi katika mfumo wake wa sheria ambao kwa hivi sasa una mapungufu yanayokwamisha kuundwa kwa mahakama hiyo maalumu.

Umoja wa Mataifa uliidhinisha mpango huo wa utafiti wa ukiukaji wa hali za binadamu nchini Congo baada ya kugunduliwa kwa makaburi matatu ya pamoja katika eneo la mkoa wa Kivu Kaskazini Mashariki mwa Congo mnamo mwaka 2005 na kuchapisha matokeo yake mnamo Oktoba 1 mwaka 2010.

Mbali na kufichua ukiukaji na unyanyasaji huo mkubwa, watafiti walitathmini uwezo wa mfumo wa haki wa Congo kwa kushughulikia kikamilifu uhalifu ulioripotiwa na kupendekeza marekebisho na njia mbadala za mifumo ya mahakama ambazo zinaweza kutoa haki na fidia. Lakini hakuna mapendekezo yoyote ya ripoti hiyo yaliyotekelezwa na hatua za adhabu bado hazijachukuliwa dhidi ya waliofanya uhalifu huo.