1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Kiarabu yakata uhusiano na Qatar

Mohammed Khelef
5 Juni 2017

Katika hali ya kushangaza, mataifa kadhaa ya Kiarabu yamekata mahusiano ya kidiplomasia na Qatar, sambamba na kuizuilia njia zote za usafiri na kuifukuza kwenye muungano dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen.

https://p.dw.com/p/2e7zl
Katar Emir Scheich Tamim bin Hamad Al-Thani
Picha: picture-alliance/AP Photo/O. Faisal

Taarifa ya hivi punde kutoka mjini Doha zinasema serikali ya Qatar imesikitishwa na hatua za Bahrain, Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Kiarabu, Yemen na Misri kuikatia mahusiano yote ya kidiplomasia kwa tuhuma za kusaidia ugaidi na kuingilia mambo ya ndani kwenye mataifa hayo.

Kituo cha televisheni cha al-Jazeera kimeinukulu wizara ya mambo ya nje ya Qatar ikisema "hatua hizo hazina mashiko na zimejikita kwenye madai na uzushi usio msingi," huku serikali ikiwahakikishia wananchi kuwa uamuzi huo hautakuwa na athari mbaya kwao.

Hata hivyo, katika uamuzi huo uliotangazwa mfululizo na nchi hizo tano alfajiri ya leo (Juni 5), serikali za mataifa hayo ya Kiarabu zimeamua kuvunja mahusiano yote ya kidiplomasia, kijeshi na kiraia, ambapo Bahrain na Saudi Arabia, kwa mfano, zimewaagiza raia wa Qatar walioko huko, kuondoka ndani ya wiki mbili kutoka sasa.

"Raia wa Saudia wanapigwa marufuku kwenda, kuishi ama kusafiri kwa ndege kupitia Qatar. Na kwa wageni na wakaazi kwenye nchi hiyo, wana siku 14 za kuondoka huko. Na bahati mbaya, kwa sababu za kiusalama na hatua za tahadhari, raia wa Qatar wanapigwa marufuku kuingia, kupitia Ufalme wa Saudi Arabia na wageni na wakaazi wanapewa siku 14 kuondoka hapa", lilisema tangazo la Saudia kwenye televisheni ya nchi hiyo.

Mashirika ya ndege yakatisha safari 

Saudi Arabien König Salman Bin Abdul Aziz Al Saud
Mfalme Salman Bin Abdul Aziz Al Saud wa Saudi ArabiaPicha: Picture alliance/abaca/B. Press

Saudi Arabia sio tu inaondosha mabalozi wake na kufunga ofisi zake mjini Doha, bali pia imeamuru mara moja kikosi cha wanajeshi wa Qatar kwenye muungano wa kijeshi nchini Yemen kiondoke. 

Shirika la ndege la Etihad, lenye makao yake makuu mjini Dubai, limetangaza hapo hapo kufuta safari zake zote nchini Qatar na bado haijawa wazi endapo Saudi Arabia italiruhusu shirika la ndege la Qatar Airways kupitisha ndege zake kwenye anga la nchi hiyo, kwa vile safari zake zote lazima zipitie kwenye anga hilo.

Mashirika mengine mawili ya ndege ya Muungano wa Falme za Kiarabu, Emirates na FlyDubai, yamekatisha safari muda mchache baada ya tangazo la serikali yao dhidi ya Qatar.

Qatar itakayokuwa mwenyeji wa mashindano ya fainali za Kombe la Dunia la Soka hapo mwaka 2022, ina kituo kikubwa cha kijeshi cha Marekani katika mataifa ya Ghuba.

Iran, Marekani zakosoa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson, ameyataka mataifa hayo kuendelea kuwa wamoja na kuzungumza tafauti zao, bila kuingia kwenye mzozo wa kidiplomasia. 

Iran Präsident Hassan Rohani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.Picha: Getty Images/AFP/A. Kenare

"Kwa hakika, tunazishajiisha pande zote kukaa pamoja, kuzungumzia tafauti baina yao. Ikiwa kuna lolote tunaloweza kufanya kuwasaidia kuyaelezea matatizo hayo, tunadhani ni muhimu kwa Baraza la Ushirikiano la Ghuba, kuwa kitu kimoja," amesema Tillerson akiwa ziarani Australia.

Kwa upande wake, Iran, ambayo inaonekana kuwa moja ya sababu za mataifa hayo ya Ghuba kuisusia Qatar, imesema uamuzi huo wa majirani zake si suluhisho la mzozo uliopo.

Hata kabla ya hatua hii ya leo, Qatar ilishaonekana kuwa kwenye mzozo na majirani zake, ikituhumiwa kutumia vyombo vyake vya habari kuchafua heshima ya mataifa hayo.

Mnamo tarehe 27 Mei, kiongozi wa Qatar, Emir Tamin bin Hamad Al Thani, alimpigia simu Rais Hassan Rouhani wa Iran kumpongeza kwa kuchaguliwa tena. 

Hatua hiyo ilichukuliwa kama ukaidi wa wazi wa Qatar dhidi ya juhudi za Saudi Arabia za kulitenga taifa hilo la Kishia, linalochukuliwa na mataifa kadhaa ya Kisunni kama adui Nambari 1. 

Tayari hisa za Qatar kwenye soko la dunia zimeshuka kwa asilimia 5.7, muda mchache tu baada ya uamuzi huo wa kukatiwa mahusiano na majirani zake, huku kampuni ya simu ya Vodafone Qatar ikipoteza asilimia 8.9 na Benki Kuu ya Taifa ikipoteza asilimia 4.6.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba