1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Magharibi yataka maafikiano ya haraka Sudan

Sylvia Mwehozi
22 Mei 2019

Marekani, Uingereza na Norway zimeitolea wito Sudan wa kupatikana makubaliano ya haraka  kati ya waandamanaji nchini Sudan na viongozi wa kijeshi kuhusu kuundwa serikali ya kiraia.

https://p.dw.com/p/3ItmJ
Sudan Khartum Proteste gegen Militär-Regierung
Picha: AFP/M. El-Shahed

Mazungumzo baina ya viongozi wa waandamanaji na wale wa kijeshi waliochukua mamlaka baada ya kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir kuondolewa madarakani, yalikwama tangu Jumatatu jioni kufuatia kutoelewana  juu ya nani ataongoza serikali, wanajeshi au raia.

Mataifa hayo ya magharibi, ambayo awali yalihusika na mazungumzo ya upatanishi katika migogoro ya Sudan, yamesema nchi hiyo "inahitaji makubaliano ya haraka ili kumaliza kipindi cha hali ya sintofahamu", kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa siku ya Jumanne. Lakini wananchi wanaonekana kuwa na maoni tofauti kuhusiana na mkwamo uliopo, Abu Baker Abdullah ni muandamanaji na anasema "ni muhimu kwa wasudan wote kuzidisha uasi wa kiraia. watu wa Sudan lazima watoke kama walivyofanya Aprili 6 ili kuweka shinikizo zaidi kwa baraza la kijeshi ili kutupatia sisi mamlaka kamili". 

Taarifa ya mataifa hayo imesema uamuzi wowote ambao hautapelekea kuundwa serikali itakayoongozwa na raia, itakayowapa raia mamlaka ya kutawala, haitakuwa imetimiza matakwa yaliyowekwa wazi na watu wa Sudan ya kutaka utawala wa kiraia.

Sudan Proteste in Khartum
Waandamanaji wanaendelea na maandamano nchini SudanPicha: Reuters/M.N. Abdallah

Aidha taarifa hiyo imeongeza zaidi ikisema "hali hiyo itafanya vigumu ushiriki wa kimataifa na kuzifanya nchi zetu kuhindwa kufanya kazi na utawala mpya sambamba na kuunga mkono maendeleo ya kiuchumi ya Sudan", ilisema taarifa hiyo iliyochapishwa katika ukurasa wa Facebook wa ubalozi wa Marekani mjini Khartoum.

Marekani mara kadhaa imesisitiza juu ya utawala wa kiraia nchini Sudan tangu Bashir aondolewe na jeshi Aprili 11 baada ya miezi kadhaa ya maandamano ya nchi nzima dhidi ya utawala wake wa miaka 30. Pia imeahirisha mazungumzo na Khartoum kwa ajili ya kuiondoa Sudan katika orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi. Hiyo ilikuwa sababu muhimu ambayo kwa miongo kadhaa imekuwa ikitia wasiwasi uwekezaji wa kigeni katika taifa hilo la Kaskazini mashariki mwa Afrika.

Viongozi wa waandamanaji nchini Sudan hivi sasa wanaandaa mipango ya maandamano makubwa kwa ajili ya kuwashinikiza zaidi majenarali wa kijeshi ili waachie madaraka. Baraza la kijeshi linalotawala limekuwa likihimiza kuwa mwenyekiti wake Jenerali Abdel Fattah al-Burhan aongoze serikali mpya jambo linalogomewa na viongozi wa waandamanaji wanaotaka kiongozi wa kiraia.

Iwapo chombo kipya cha utawala kitakapokamilika kinatarajiwa kuanzisha serikali ya kiraia ya mpito kwa miaka mitatu na baadae kufanya uchaguzi wa kwanza baada ya Bashir kuondolewa.